
Mkuu wa Wilaya ya
Simanjiro Mkoani Manyara mhandisi Zephania Chaula akishiriki kukata
utepe na wadau wa madini kwenye uzinduzi wa soko la madini ya vito
Orkesumet.

Mkuu wa Wilaya ya
Simanjiro Mkoani Manyara mhandisi Zephania Chaula akizungumza kwenye
uzinduzi wa soko la madini ya vito Mji mdogo wa Orkesumet.

Matukio mbalimbali kwenye uzinduzi wa soko la madini ya vito Mji mdogo wa Orkesumet Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara
…………………..
MKUU wa Wilaya ya
Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula amezindua soko la
madini ya vito kwenye mji mdogo wa Orkesumet.
Soko hilo litatumika kuuza na kununua madini ya vito ikiwemo Ruby, Green Tomarine, Green Gainet, Tanzanite na mengineyo.
Mhandisi Chaula
akizungumza wakati akizindua soko hilo, amewataka wafanyabiashara na
wachimbaji wa madini kutumia soko hilo kuuza madini na kulipa kodi ya
serikali.
Chaula alisema
serikali imelenga kuondoa ukiritimba kwenye sekta ya madini hivyo
wachimbaji na wanunuzi watumie fursa hiyo kwa kuuza na kununua madini
kwenye soko hilo.
“Baada ya kumaliza
uzinduzi wa soko hilo la madini Orkesumet tutazindua soko lingine
Mirerani hivyo kuwa na masoko mawili kwenye mkoa wa kimadini wa
Simanjiro hiyo ni hatua kubwa mno,” alisema mhandisi Chaula.
Aliwataka
wafanyabiashara na wachimbaji kutumia masoko hayo kulipa kodi kwani
ndizo zinazotumika kwenye maendeleo mbalimbali ya jamii.
“Mnaona pale
tunajenga hospitali ya wilaya ya Simanjiro, awali hatukuwa nayo ila
kupitia makusanyo ya ndani yanayotokana na kodi zenu na usimamizi wa
Rais John Magufuli hivi sasa tumekamilisha hospitali,” alisema mhandisi
Chaula.
Mwenyekiti wa chama
cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (Marema) Justin Nyari alimpongeza
mkuu huyo wa wilaya na ofisi ya madini kwa kuhakikisha soko hilo
linafanikishwa kuanzishwa ili kutimiza agizo la Rais John Magufuli.
Nyari alisema
wanamuomba mkuu huyo wa wilaya kupeleka salamu zao kwa mkuu wa Mkoa huo
Alexander Mnyeti ili azifikishe kwa Rais John Magufuli kwani anawapenda
na kuwapa kipaumbele wachimbaji na sekta ya madini kwa ujumla.
Kaimu ofisa madini
mkazi mkoa wa kimadini wa Simanjiro mhandisi Castro Maduwa alisema
wamejipanga kuvuka lengo la makusanyo ya kodi ya sh6 bilioni kwa mwaka
wa fedha wa 2019/2020.
Maduwa alisema mwaka jana 2018/2019 walipangiwa wakusanye sh1.5 bilioni lakini wakakusanya sh2.8 bilioni hivyo kuvuka lengo.
Katibu wa CCM wa wilaya ya Simanjiro Ally Kidunda alisema ilani ya uchaguzi wa CCM inazidi kutekelezwa kwa vitendo Simanjiro.
Makamu Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Sendeu Laizer alipongeza hatua hiyo
kwani itaongeza tija kwa wachimbaji na wanunuzi wa madini Simanjiro
No comments :
Post a Comment