
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe.Prof.Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Mkoa
wa Njombe mara baada ya kuwasili mkoani humo kuanza ziara ya Kikazi.

Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe.Prof.Ibrahim Hamis Juma,akikagua ujenzi wa jengo la mahakama ya
mwanzo Makete wilayani Makete,akiwa katika ziara ya kikazi kwenye mikoa
ya Njombe na Iringa
………………
Na Lydia Churi- Mahakama Njombe
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma leo ameanza ziara ya kikazi katika mikoa ya Iringa na
Njombe na kutaka kuwepo kwa matumizi ya vipimo vya vinasaba (DNA)
katika kesi za mauaji, ubakaji na unajisi kwa watoto ili kurahisisha
uendeshaji wa kesi hizo na
kusaidia haki kupatikana kwa wakati.
Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa
Njombe Mhe. Christopher Ole Sendeka alipomtembelea ofisini kwake, Jaji
Mkuu amesema matumizi ya vipimo vya DNA katika kesi yatasaidia haki
kupatikana ambapo aliyetenda kosa atatiwa hatiani na asiyetenda kosa
ataachiwa mapema.
“Kipimo cha DNA husaidia
kuthibitisha kosa lililofanyika lakini bahati mbaya, kwa uzoefu wetu
hatuoni matumizi ya kipimo hicho”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema kutokutumika kwa kipimo cha DNA Mahakamani, mshtakiwa huweza kuachiwa huru kutokana na kukosekana kwa ushahidi.
“Eneo hili tumeona huweza
kusababisha mtuhumiwa kuachiwa huru kwa sababu sisi tunaangallia zaidi
ushahidi” alisisitiza Jaji Mkuu.
Alisema wakati mwingine Jaji au
Hakimu huweza kuona wazi kuwa mshtakiwa alistahili kutiwa hatiani lakini
ushahidi unapokosa uzito mtuhumiwa huachiwa huru.
Akifafanua, Jaji Mkuu Alisema kesi
kama hizi huchukua muda mrefu na kusababisha wakati mwingine ushahidi
muhimu kufifia kiasi kwamba kesi inapofika mahakamani lile joto la
ushahidi lililoonekana wakati wa tukio huweza kupotea.
Alisema kutokana na kukua kwa
sayansi na Teknolojia hivi sasa hatua kubwa imefikiwa katika matumizi ya
kipimo cha DNA na kurahisisha sana. Akitolea mfano wa kesi ya ubakaji
au unajisi kwa watoto wadogo alisema badala ya kumuhoji mtoto mdogo
mahakamani, kipimo hiki huweza kutumika ili kuthibitisha kosa
lililofanyika.
Alisema Serikali kwa kushirikiana
na Mahakama hawana budi kuifanyia kazi changamoto hii ili kila raia
anayetenda kosa atiwe hatiani na asiye na kosa aachiwe huru mapema hata
katika hatua ya upelelezi wa kesi husika.
Wakati huo huo, Jaji Mkuu alisema
suala la ujazaji wa fomu za taarifa ya Daktari yaani PF 3 halizingatiwi
kwa kuwa fomu hizo hazijazwi kwa ufasaha na hivyo huweza kusababisha
mtuhumiwa kuachiwa huru wakati mwingine.
“Fomu hii inayo maeneo muhimu ya
kujazwa na hasa yanayohitaji vipimo na endapo itajazwa kwa ufasaha
itasaidia sana katika kuhakikisha mtu anayetenda kosa anatiwa hatiani”,
alisema.
Kuhusu kesi za Mirathi, Jaji Mkuu
alisema eneo hili lina changamoto kwa kuwa kesi hizi pia huchukua muda
mrefu zaidi hivyo elimu haina budi kutolewa hasa kwa wananchi wanaoishi
maeneo ya vijijini. Alisema wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa kila mtu
anapaswa kujitahidi kutafuta chake badala ya kutegemea cha marehemu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe
alimpongeza Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kujitoa kwake katika kuhakikisha
Mahakama inatoa mchango mkubwa kwenye maendeleo ya nchi na pia
alimpongeza kwa kuendeleza ushirikiano na Mihimili ya Serikali na Bunge.
Aidha, Mhe. Ole Sendeka ameahidi
kushirikiana kwa karibu zaidi na Mahakama ya Tanzania inapotekeleza
majukumu yake ya msingi ya utoaji wa haki kwa wakati.
Katika ziara iliyoanza leo, Jaji
Mkuu ametembelea Mahakama ya wilaya ya Makete na kuzungumza na watumishi
wa Mahakama hiyo lakini pia alipata nafasi ya kukagua ujenzi wa jengo
la Mahakama ya Mwanzo Makete.
No comments :
Post a Comment