Naibu
Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi),
Elias Kwandikwa, akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Miundombinu, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mjini Dodoma.


……………………………..
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Miundombinu imeupongeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kwa
utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madaraja makubwa na barabara ya
kuunganisha mkoa kwa mkoa kupitia mtandao wa barabara nchini.
Akizungumza mara baada ya kupokea
taarifa ya utekelezaji ya Wakala huo ilyowasilishwa
kwa Wajumbe wa
Kamati jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Selemani Kakoso,
amesema kuwa kupitia utaratibu huo hata barabara zilizosahaulika nchini
zinaweza kunufaika kwa kuwa na maendeleo ya kiuchumi kutokana na uwepo
wa miradi hiyo.
“Naipongeza Serikali kupitia
TANROADS kwa kufikiria kuunganisha mikoa kupitia barabara hususan katika
mikoa ya Katavi, Rukwa, Kigoma na Kagera. Mikoa hii ilionekana kama
imesahaulika lakini sasa inaonekana kupata maendeleo kutokana na uwepo
wa miradi ya barabara ambayo inatekelezwa”, amesema Mhe. Kakoso.
Aidha, Ameutaka Wakala huo
kuendelea kuziangalia na kuzipa kipaumbele barabara za kimkakati ambazo
zina maslahi mapana katika maendeleo na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Ametaja miradi hiyo kama barabara
ya Mtwara- Mnivata, Katavi- Kigoma na Kasulu – Kagera ambayo kwa pamoja
ikikamilika itaunganisha mikoa hiyo na mikoa jirani na hatimaye kufungua
fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Mwenyekiti Kakoso, ameusisitiza
Wakala huo kuendelea na uboreshaji wa viwanja vya ndege hususan katika
ujenzi wa majengo ya abiria ambayo yanaendana na wingi wa abiria pamoja
na kujenga uzio katika viwanja vya ndege ambavyo havina uzio lengo
likiwa ni kuweka usalama katika viwanja hivyo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elias
Kwandikwa, amesema kuwa Serikali itaendelea kutekeleza ujenzi na
ukarabati wa barabara, madaraja na mizani.
Amefafanua kuwa hadi kufikia Juni,
2019 Wakala umefanikiwa kujenga kituo cha mizani cha Kurasini ambacho
kimejengwa kwa ajili ya kuhakiki uzito wa magari yanayotoka bandarini
na kuweka CCTV Kamera katika mzani huo.
Kwandikwa, ameongeza kuwa Wakala
umeendelea na kazi za ujenzi na ukarabati wa miradi mbalimbali ya
viwanja vya ndege ambapo hatua za utekelezaji zilizofikiwa kwa baadhi ya
miradi zinaridhisha.
Amesema kuwa hadi kufikia Juni,
2019 ujenzi wa Jengo la abiria katika Kiwanja cha ndege wa Songwe
umefika asilimia 77 na ukarabati na ujenzi wa Jengo la kuongozea ndege
na mizigo katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza umefika asilimia 93.
“Sisi kama Serikali tutaendelea
kuboresha viwanja vingine vya ndege, tunajua wananchi wanahitaji
maendeleo kupitia sekta ya anga, hivyo hatuna budi kuboresha viwanja
hivi, amesisitiza Kwandikwa.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Miundombinu imepokea taarifa ya TANROADS ambayo imeainisha majukumu ya
Wakala huo kwa mwaka wa Fedha 2018/19 na utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi na ukarabati wa barabara kuu,
barabara za mikoa, madaraja na viwanja vya ndege.
No comments :
Post a Comment