Na Veronica Simba - Chato
Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewaasa wananchi wa Kitongoji cha
Mwamagili, Wilaya ya Chato, mkoani Geita kutumia umeme aliowawashia
rasmi jana, Juni 30, 2019 kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya
kimaendeleo.
Akizungumza
na wananchi hao muda mfupi kabla ya kuwasha umeme katika nyumba ya
mkazi wa kitongoji hicho, Kashonele Kagodoro, Dkt. Kalemani aliwaambia
endapo watautumia ipasavyo, hali zao za maisha zitaboreka zaidi.
“Umeme
huu siyo kwa ajili ya kuwasha taa peke yake. Anzisheni miradi
mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo mashine za kukoboa na kusaga nafaka,
saluni za kike na kiume na miradi mingine mbalimbali ili kuinua kipato
chenu hivyo kuboresha maisha yenu.”
Aidha,
Waziri Kalemani ambaye pia ni Mbunge wa eneo hilo (Chato), aligawa
vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) kwa nyumba zote 38 za kitongoji hicho,
ambazo zilikuwa bado hazijaunganishiwa umeme ikiwa ni sehemu ya
kuwahamasisha wananchi husika kulipia gharama ndogo ya shilingi 27,000
tu ili waunganishiwe nishati hiyo.
“Kwa
kutumia kifaa hiki cha UMETA, mtaepuka gharama za kutandaza nyaya
katika nyumba zenu. Niwaombe na kuwahamasisha muendelee kulipia kwa
sababu bei ya kuunganishiwa umeme ni ndogo sana; shilingi 27,000 tu,”
asisitiza Waziri.
Katika
hatua nyingine, Waziri amelipia gharama za kuunganisha umeme katika
Kanisa lililopo eneo hilo, ambayo pia ni sehemu ya kuhamasisha viongozi
wa taasisi mbalimbali za umma kulipia gharama za umeme ili ziunganishwe.
Wananchi
kadhaa waliopata fursa ya kueleza maoni yao mbele ya Waziri Kalemani,
walipongeza jitihada za Serikali katika kuwapelekea nishati ya umeme.
“Hii
ni ndoto kwangu. Sikutegemea. Tangu nizaliwe nilikuwa nikiona umeme
maeneo ya mijini nilikowahi kutembelea. Sikuwahi kuwaza kuwa iko siku
umeme utawashwa kijijini kwetu, tena katika nyumba yangu,” alisema
Kagodolo.
Waziri Kalemani yuko Chato kwa ziara ya kazi.
No comments :
Post a Comment