Tanzania
na Nchi ya Falme za Kiarabu zimekubaliana kuendelea kuimarisha
mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi ikiwa ni pamoja na kushirikiana
katika masuala ya usalama wa eneo la Ghuba na bahari ya Hindi pia
kusaidia kuimarisha hali ya usalama katika nchi za Somalia na Sudan.
Hayo
yamebainika wakati wa ziara ya Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi alipomtembelea na
kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Umoja wa
Falme za kiarabu Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan.
Katika
Mazungumzo hayo wawili hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha udugu wa
muda mrefu baina ya mataifa hayo mawili ikiwa ni pamoja na kufufua
mazungumzo ya Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) ambayo kwa
mara ya mwisho yalifanyika katika Mji wa Abu Dhabikatika Umoja wa Falme
za Kiarabu ili kufufua na kutekeleza makubaliano ikiwa ni pamoja na
kuangalia fursa za kiuchumi kwa faida ya pande zote mbili.
Akizungumza
mara baada ya mazungumzo hayo Waziri Palamgamba John Kabudi amesema
pamoja na masuala mbalimbali waliyokubaliana pia Waziri wa Mambo ya Nje
wa Serikali ya Umoja wa Falme za kiarabu Sheikh Abdullah bin Zayed Al
Nahyan ameahidi kufanya mazungumzo na Ubalozi wa Falme za Kiarabu uliopo
Nchini Tanzania ili kuharakisha matayarisho ya Ubalozi huo kuhamia
Dodoma baada ya serikali ya Tanzania kuupatia ubalozi huo eneo la
kujenga ubalozi wa Nchi hiyo mjini Dodoma bure.
Waziri
Kabudi ameongeza kuwa mazungumzo hayo yamekuwa ya manufaa kwa pande
zote mbili na kwamba yataendelea kuimarisha mahusiano baina ya Nchi hizo
mbili ikiwa ni pamoja na kufungua fursa za kibiashara kwa ajili ya
maendeleo ya mataifa hayo.
Katika
hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Prof Palamagamba John Kabudi akizungumza wakati akihitimisha
ziara yake Nchini China,amesema ziara hiyo imekuwa ya manufaa kiuchumi
kwa Tanzania ambapo tayari wawekezaji takribani 150 wanatarajiwa
kuwasili nchini Tanzania kwa nia ya kuangalia maeneo mbalimbali ya
uwekezaji mapema mwezi septemba wakitanguliwa na ujumbe wa watu 10 mwezi
Julai 2019,hii ikiwa ni kipindi kifupi sana mara baada ya Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhudhuria mkutano wa
kwanza wa maonesho ya uchumi na biashara kati ya China na Afrika
uliofanyika katika mji wa Chanshang katika jimbo la Hunan,Nchini China.
Aidha
ametanabaisha kuwa tayari wamepatikana wawekezaji wanaotaka kujenga
nyumba ya kulala wageni yenye vyumba mia tatu katika mji wa Karatu
ulioko mkoani Manyara kwa nia ya kuhamasisha watalii hususani kutoka
China ambao wanatarajiwa kuongezeka maradufu kufuatia hatua ya Tanzania
kuweka msisitizo katika kutangaza vivutio vyake vya Utalii.
Pia
Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Beijing kimekubali ombi la Waziri Kabudi
la kutaka kuongeza idadi ya wanafunzi watakaokwenda kusoma chuoni hapo
kutoka 20 hadi kufikia idadi 40 nafasi zitakazotolewa kwa ufadhili wa
chuo hicho kila mwaka ili kuandaa nguvu kazi ya kutosha wakati Tanzania
ikijiandaa kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
No comments :
Post a Comment