Thursday, July 11, 2019

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI (NEC) YAVITAKA VYAMA VYA SIASA VIACHE KUPELEKA MALALAMIKO KATIKA VYOMBO VYA HABARI



Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vya siasa nchini kutopeleka malalamiko yao katika vyombo vya habari kuhusu masuala ya uchaguzi na badala yake viwasilishe hoja hizo katika Kamati za Maadili za Uchaguzi.

Imesema haina mfumo wa kushughulikia malalamiko ya uchaguzi kupitia vyombo vya habari badala yake imetaka utaratibu wa kisheria kufuatwa ili haki itendeke kwa wote. 

Mkurugenzi wa NEC, Dk Athuman Kihamia alisema hayo akiwasilisha mada ya Uboreshaji daftari la kudumu la wapigakura katika semina ya viongozi wa vyama vya siasa, dini, walemavu, vijana, wanawake, asasi za kiraia na watendaji wa NEC.

‘’Pamoja na uwepo wa Kamati za maadili zenye mamlaka ya kutatua migogoro na kuweka mazingira sawa ya ushindani katika chaguzi ndogo, vyama vimekuwa havipeleki malalamiko yao kwenye kamati hizo bali hutoa malalamiko yao kupitia vyombo vya habari, ‘’ alisema. 

Alizitaja kamati zinazoundwa wakati wa uchaguzi kuwa za maadili ya uchaguzi, kamati ya rufaa, kamati ya maadili ya kitaifa, kamati ya maadili ya jimbo na kamati ya maadili ya kata.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage alisema kifungu cha 15 (5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343 kikisomwa na kifungu cha 21 (5) cha Sheria ya uchaguzi ya serikali za mitaa kinaipa NEC mamlaka kuboresha daftari la kudumu la wapigakura.

Alisema pia NEC iliendesha uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapigakura nchini ambapo kwa mkoa wa Kilimanjaro, iliongeza vituo vya kujiandikisha kutoka vituo 1,273 hadi 1,286

No comments :

Post a Comment