Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kukusanya jumla ya TZS 15.9
trilioni kati ya lengo la TZS 18 trilion kwa mwaka wa Fedha 2018/19
kuanzia tarehe 1 Julai 2018 hadi 30 Juni 2019. Aidha katika robo ya nne
ya mwaka huo wa fedha yaani, mwezi Machi hadi Juni 2019, TRA ilikusanya
TZS 1.1 trilioni, TZS 1.2 trilioni, na TZS 1.5 trilioni kwa mwezi
Aprili, Mei, na Juni, mtawalia. Kwa namna ya kipekee kabisa, TRA
inawashukuru walipakodi na wananchi wote kwa ujumla kwa ushirikiano.
Ikumbukwe kwamba, katika mwaka huo wa fedha, Serikali ilianzisha Mfumo
wa Stempu za Kodi za Kielektroniki (ETS) ambao utekelezaji wake
umefanyika kwa awamu mbili (2). Awamu ya kwanza, ilihusisha bidhaa za
sigara, mvinyo, pombe kali, bia na aina zote za vileo. Awamu hii ya
kwanza iliyoanza kutekelezwa tarehe 15 Januari 2019 imeendelea vizuri na
maandalizi ya awamu ya pili ya utekelezaji wa ETS inayojumuisha bidhaa
za vinywaji baridi, maji, juisi, na CD/DVDs yamekamilika. Hivo mfumo huu
wa ETS kwa awamu hii ya pili, unatarajiwa kuanza kazi rasmi tarehe 1
Agosti, 2019.
Lengo kuu la kubandika stempu hizi za kielektroniki ni kuongeza
usimamizi na ufanisi wa ukusanyaji wa Ushuru wa bidhaa ikiwa ni pamoja
na kupata taarifa sahihi za uzalishaji viwandani ili kukusanya mapato
stahiki.
Ni matumaini ya TRA kuwa, wazalishaji, waingizaji, wasambazaji, wauzaji
wote wa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa pamoja, na umma kwa ujumla
wataendelea
kutoa ushirikiano kwa TRA ili kufanikisha utekelezaji wa mfumo huu kwa
kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu
zilizopo.
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”
Richard M. Kayombo
KAIMU MKURUGENZI WA HUDUMA NA ELIMU KWA MLIPAKODI
No comments :
Post a Comment