Na. Mwandishi Wetu.
Serikali
kupitia Idara ya Uhamiaji imetoa ufafanuzi kuhusu Mwandishi wa
kujitegemea Erick Kabendera baada ya kusambaa kwa taarifa kwenye vyombo
vya habari na mitandao ya kijamii, kuwa amekamatwa na anahojiwa kuhusu
uraia wake na Idara ya Uhamiaji Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
Jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Uraia na Pasipoti wa Idara ya
Uhamiaji Gerald Kihinga, amesema kuwa Erick Kabendera ameshikiliwa na
Jeshi la Polisi na Uhamiaji Jijini Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi ili
kuweza kupata taarifa juu ya uraia wake.
Kamishna
huyo wa Uhamiaji amesema Idara ya Uhamiaji inadhamana kubwa ya
kusimamia na kutekeleza Sheria ya uraia wa Tanzania sura ya 357 rejeo la
2002, inayotoa mamlaka kwa taasisi hiyo kuchunguza na kuthibitisha
uraia wa mtu yeyote.
“Idara
ya Uhamiaji ni chombo kilichopewa dhamana kubwa ya kutekeleza na
kusimamia uraia wa Tanzania, kwa hiyo siyo mara ya kwanza kufanya hivyo,
sisi tunamshikilia Kabendera kwa mahojiano kuhusu uraia wake, na siyo
yeye tu aliyefanyiwa hivyo, idara ya Uhamiaji inatimiza matakwa ya
sheria ya uraia nchini na wala si vinginevyo” Alisema.
Alieleza
kuwa idara ya Uhamiaji ilipata taarifa za Erick Kabendera kutoka kwa
raia wema na ikaamua kumtafuta ili kufanya naye maojiano lakini hakuwa
tayari kutoa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kukataa kufika ofisi za
Uhamiaji, hali iliyopelekea kukamatwa na sasa anaendelea kuhojiwa.
Mkuu
huyo wa masuala ya uraia na Pasipoti alifafanua kuwa, kushikiliwa huko
kwa Erick Kabendera na kuendelea na mahojiano ni swala ambalo limekuwepo
kwa raia wote ambao uraia wao una utata, wakiwemo watu wa kawaida,
watu mashuhuri na wengine wowote ambao kutaonekana uhitaji.
Amesema
kumekuwa na ushirikiano baina ya Uhamiaji na vyombo vingine vya ulinzi
na usalama ikwemo Polisi, ili kutekeleza majukumu mbalimbali ya
kiusalama kwa nchi hivyo kukamatwa kwa Kabendera siyo jambo geni bali
Idara inatimiza majukumu yake chini ya Sheria ya uraia wa Tanzania sura
ya 357 rejeo la 2002.
No comments :
Post a Comment