
Jeshi
la Wananchi (JWTZ) limetangaza kuwachukulia hatua viongozi wa ndani na
nje ya jeshi hilo na vijana waliohusika katika vitendo vya udanganyifu
katika uandikishaji wa majina ya kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT).
Udanganyifu huo ulihusisha ukiukaji wa taratibu na kughushi nyaraka na vyeti vilivyotumika katika uandikishaji huo.
Mkurugenzi
wa Habari na Uhusiano JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda,
akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo, alisema licha ya taratibu za
uombaji kuwa wazi, baadhi ya viongozi wamebainika kutumia nafasi
walizonazo kupenyeza majina ya ndugu, jamaa na rafiki ili wasajiliwe.
“Napenda
kuwataarifu kuwa baada ya kubaini kuwako kwa udanganyifu huu, JWTZ/ JKT
tutafanya uhakiki wa vyeti na nyaraka zote husika kwa vijana
walioandikishwa tutashirikiana na ofisi ya Nida (Mamlaka ya Vitambulisho
vya Taifa), Baraza la Taifa la Mitihani, Takukuru na vyombo vingine vya
ulinzi na usalama ili kuwabaini waliofanya udanganyifu,” alisema Kanali
Ilonda.
Ilonda
bila kutaja uhakiki huo utafanyika lini na wakati gani, alisema
utahusisha kuhakiki wa vyeti, nyaraka mbalimbali zilizokuwa zikihitajika
kwenye uandikishaji huo pamoja na vyeti vya kuzaliwa na vipimo vya
afya.
"Kwa
kuweka usawa tutafanya uhakiki huu kwa kushirikiana na JKT, Nida,
Wizara ya Elimu, taasisi zinazohusika na masuala ya rushwa, vyombo vya
ulinzi na usalama, ili tuweze kuwachuja, tunataka kujiridhisha je, ni
Watanzania kweli, wana afya njema, wana akili timamu, ametoka eneo
husika na ana sifa stahiki, wale wenye sifa watachukuliwa, hata kama
idadi yao itakuwa ndogo tofauti na matarajio yetu," alisema.
Ilonda alisema wale ambao watabainika kughushi watakamatwa na kufunguliwa mashtaka.
“Hakuna
atakayesalimika labda wahame nchi, aliyeghushi vyeti na nyaraka
mbalimbali kiwe cha kuzaliwa au daktari aliyetoa majibu ya uongo
atakamatwa, waliowashawishi kughushi watakamatwa, waliotengeneza vyeti
bandia, waliohusika kuwaandikisha vijana hao bila kuwa na vigezo,
viongozi wote waliohusika kupenyeza majina wa ndani na nje ya jeshi nao
watachukuliwa hatua kupitia mamlaka zao husika,” alisema.
Alisema
hatua zitakazochukuliwa hazitaangalia wadhifa au cheo cha mtu kwa
sababu lengo ni kusafisha nchi iwe na viongozi waadilifu na wanaofuata
sheria na taratibu.
No comments :
Post a Comment