Askari
Polisi wawili na mfanyakazi mmoja wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA),
waliotajwa na mfanyabiashara Ikulu kwamba wamemdai rushwa na kuzuia
mzigo wake tangu mwaka 2016 wamepandishwa kizimbani.
Mfanyabiashara
huyo aliwataja katika mkutano wa Rais Dk. John Magufuli na
wafanyabiashara uliofanyika Juni 7, mwaka huu ikulu jijini Dar es
Salaam.
Washtakiwa
hao wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo
Juni 10, kwa tuhuma za kushawishi kupewa rushwa ya Sh milioni mbili na
mfanyabiashara Ramadhan Ntuzwe.
Washtakiwa
ambao ni askari na namba zao ni H 4086 PC Simon Sungu, H 4810 PC
Ramadhan Uwezi wa Kituo cha Polisi Osterbay na Mfanyakazi wa TRA,
Charity Ngalawa.
Wakili
wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
Sophia Gula aliwasomea washtakiwa shtaka linalowakabili mbele ya Hakimu
Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Amedai
washtakiwa wanashtakiwa kwa kushawishi rushwa, wanadaiwa Oktoba 29,
2016 maeneo ya Kimara mwisho, wakiwa wafanyakazi wa TRA na Polisi
walidai rushwa ya Sh milioni mbili kutoka kwa Ntuzwe.
Washtakiwa
wanadaiwa walidai rushwa hiyo kama kishawishi cha kuruhusu mzigo wake
ambao unadaiwa ulikadiriwa kodi ndogo jambo ambalo lilikuwa chini ya
wakubwa wao.
Washtakiwa
walikana kutenda makosa hayo, Jamhuri walidai upelelezi haujakamilika
na hapakuwa na pingamizi kwa washtakiwa kupata dhamana.
Mahakama
ilikubali kuwapa dhamana kwa masharti ya kuwa na mdhamini mmoja
atakayesaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni tano, washtakiwa
walitimiza masharti wako nje kwa dhamana.
No comments :
Post a Comment