Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari
KwaMtoro wilayani Chemba mkoani Dodoma, Bi. Neema Muna (mwenye miwani),
akieleza changamoto zinazoikabili shule hiyo kwa Wahandisi wanawake
kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi),
Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara,
walipofika shuleni hapo kuhamasisha umuhimu wa usomaji wa masomo ya
Sayansi na Hisabati kwa wasichana.
Mhandisi kutoka Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha
ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara, Bi. Upendo Sanze,
akielekeza jambo kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya KwaMtoro
wilayani Chemba mkoani Dodoma, kuhusu umuhimu wa masomo ya Sayansi na
Hisabati.
Mwanafunzi Siminza Mambo, kutoka
Shule ya Sekondari ya KwaMtoro wilayani Chemba mkoani Dodoma, akitoa
maoni kwa Wahandisi wanawake kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) walipofika shuleni hapo kuhamasisha
usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa wasichana.
Maabara ya Shule ya Sekondari ya
KwaMtoro wilayani Chemba mkoani Dodoma licha ya kukamilika lakini bado
inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vifaa.
Wahandisi wanawake kutoka Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha
ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara, wakiwa katika picha
ya pamoja na wanafunzi pamoja na walimu wa Shule ya Sekondari ya
Dalai, wilayani Kondoa mkoani Dodoma mara baada ya kutoa elimu ya
umuhimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa wanafunzi hao.
Picha na WUUM
…………………….
Na Siti Said
Wahandisi wa kike wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), kupitia Kitengo
maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara,
wamewataka
wanafunzi wa kike mkoani Dodoma, kuchangamkia fursa za
usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati ili kuongeza wataalam katika
fani ya Uhandisi.
Akizungumza kwa niaba ya wahandisi
hao katika shule ya Sekondari ya KwaMtoro, Wilayani Chemba mkoani
Dodoma, Mhandisi Rahma Mwinyi , amesema kuwa sekta hiyo bado ina uhaba
wa wataalamu wa kike hivyo inahitaji wanafunzi kusoma masomo hayo ili
kuongeza idadi ya wataalamu hao na kuweza kufikia uchumi wa viwanda
ifikapo 2025.
“ Hakikisheni mnasoma masomo ya
Sayansi na Hisabati kwa bidii, ufaulu wa masomo haya utategemea
ufanyaji wa maswali na mazoezi ya kujipima mara kwa mara ambayo
yatawajengea uelewa na kupelekea kufaulu vizuri, Serikali bado inahitaji
wataalam wa fani hii na pia fursa za ajira kupitia fani hii zipo
nyingi, kazi kwenu kujipanga ili mfikie malengo yenu”, amesema Mhandisi
Mwinyi.
Aidha, Mhandisi Mwinyi amewataka
wanafunzi hao kuachana na dhana potofu ya kuwa masomo hayo ni magumu na
badala yake kutafuta njia mbadala ikiwemo ya kupanga ratiba ya masomo
yao vizuri na kuzingatia yale wanayofundishwa na walimu darasani.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule
ya Sekondari ya KwaMtoro, Bi. Neema Muna, kwa niaba ya walimu wenzake
ameishauri Serikali kuhakikisha wanapeleka vifaa vya maabara kwa shule
ambazo hazina vifaa hususan vijijini kwani ufaulu wa masomo hayo
hutegemea sana kufanya mazoezi kwa vitendo.
Ameongeza kuwa ipo haja ya
Serikali kuajiri na kupeleka walimu wa kutosha katika shule zilizopo
vijijini kulingana na idadi ya wanafunzi na pia huduma za maji na umeme
ziboreshwe ili kukidhi mahitaji ya ufanyaji wa mazoezi kwa vitendo
kupitia katika maabara zao.
Naye, Mwanafunzi Siminza Mambo wa
shule hiyo, ameiomba Serikali kuongeza walimu wa kike wa sayansi shuleni
hapo kwani kwa sasa shule hiyo ina mwalimu mmoja tu wa jinsia hiyo hali
inayowakatisha tamaa wanafunzi wa kike kujiunga na masomo hayo.
Pia, Mwanafunzi Lucy Isack, kutoka
shule hiyo ameiomba Serikali kuongeza walimu wa sayansi na hisabati,
vitabu na kuboreshea miundombinu ya maabara ikiwemo vifaa vya kupimia
kemikali.
Ziara ya wahandisi hao katika
shule mbalimbali za Sekondari za mkoa wa Dodoma inalenga kuhamasisha
usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa wasichana ambapo leo
wametembelea shule ya KwaMtoro, Dalai na Mondo.
No comments :
Post a Comment