Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
DAR ES SALAAM
RAIS Dkt. John Pombe Magufuli ametoa
siku saba kwa Wakuu wa Mikoa inayozalisha dhahabu nchini kushirikiana na
Wizara ya Madini katika kufungua masoko ya madini ikiwemo dhahabu ili
kuifanya sekta ya madini kuweza kuleta tija ya kiuchumi kwa Watanzania
wote hususani wachimbaji wadogo.
Akizungumza Mkoani Mbeya leo Jumamosi
(April 27, 2019) wakati wa katika hafla ya uzinduzi na
uwekaji wa jiwe
la msingi la barabara ya Mbeya-Lwanjilo-Chunya-Makongosi yenye urefu wa
Kilometa 111, Rais Magufuli alisema Serikali anayoiongoza kamwe
haitokubali kuona wachimbaji wadogo wakiendelea kuteseka nchini.
Aliongeza kuwa tangu mwaka 2017, Serikali
imepitisha Sheria Bungeni inayotoa maelekezo kuhusu usimamizi wa sekta
ya madini nchini na hivyo anashangwa na baadhi ya Viongozi wake hususani
Wakuu wa Mikoa inazozalisha dhahabu kusuasua katika kusimamia maelekezo
ya maelekezo yake aliyoyatoa katika siku za nyuma.
Alisema kuwa Serikali pia imefuta kodi
mbalimbali za madini na kuendelea kuwahamasisha wachimbaji wadogo
kupeleka dhahabu zao katika masoko hayo, lakini hadi sasa baadhi ya
Wakuu wa Mikoa wameshindwa kujenga masoko hayo, pamoja na faida
mbalimbali zinazopatikana katika masoko hayo ikiwemo kuepusha dhuluma
kwa wachimbaji, kupata dhahabu yenye ushindani pamoja na kuzuia upotevu
wa kodi ya Serikali.
Aliongeza kuwa katika mkutano wake
alioufanya hivi karibuni na Viongozi wa Wizara ya Madini na Wakuu wa
Mikoa ya Tanzania Bara inayozalisha Dhababu, alitoa maelekezo ya
kufungua masoko ya madini katika maeneo yao, ingawa ni Mkoa wa Geita
pekee uliyotekeleza maelekezo hayo wakati ujenzi huo hauhitaji nyumba au
eneo kubwa.
“Kama Mkoa wa Geita, umeweza kuwa na Kituo
cha soko la kuuzia madini, nashangazwa kwanini Wakuu wengine wa Mikoa
wanashindwa kutekeleza maelekezo hayo, hivyo hili ni agizo kwa Wakuu wa
Mikoa ya Katavi, Singida na Arusha kuhakikisha kuwa watatekeleza maagizo
haya” alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alisema Serikali
anayoiongoza haiwezi kuwa na Viongozi na Watendaji wasiotaka kutekeleza
maagizo, hivyo ametoa kipindi cha muda huo kuhakikisha kuwa vituo hivyo
vinafunguliwa na hivyo kuwahakikishia masoko ya uhakika wachimbaji
wadogo ambao wamekuwa wakidhulumiwa dhahabu zao na baadhi ya
wafanyabiashara wasio waaminifu.
Aidha Rais Magufuli aliutaka Uongozi wa
Mkoa wa Mbeya hususani Wilaya ya Chunya kuhakikisha kuwa soko hilo la
dhahabu linafunguliwa haraka iwezekanavyo kwa kuzingatia kuwa rasilimali
zote muhimu za kufanikisha maagizo hayo zipo ikiwemo vyombo vya ulinzi
na usalama ambavyo vitatumika kwa ajili ya ulinzi wa madini ya dhahabu
wakati wa mauzo hayo yakifanyika.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, alisema kuwa
suala la kujiletea maendeleo kwa Watanzania linacheleweshwa na baadhi ya
Viongozi Watendaji Serikali kwani wananchi hususani wachimbaji wadogo
wa madini wamekuwa na juhudi kubwa za kujiletea maendeleo yao lakini
wamekuwa wakikatishwa tamaa pamoja na juhudi kubwa wanazozionyesha
katika kuchimba dhahabu.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Dotto
Biteko alisema tangu kutungwa kwa Sheria ya Madini mwaka 2017, Serikali
imeweza kuokoa kiasi kikubwa cha madini kutoroshwa nje ya nchi, ambapo
katika Wilaya ya Chunya ambayo ni Wilaya ya pili kwa uzalishaji wa
dhahabu Serikali imeweza kutoa jumla ya kilo 30 zilizokuwa zikitoroshwa
nje ya nchi kutokana na kukosekana kwa mtambo wa kuchenjulia madini.
Mara baada ya kujiridhisha na taratibu
zote za kisheria, tumeweza kufungua mitambo 38 ya kuchenjulia dhahabu
hapa Chunya, ambayo tulisimamisha shughuli hizi huko nyuma kutokana na
utoroshaji mkubwa uliokuwa ukifanyika” alisema Biteko.
No comments :
Post a Comment