Na Emmanuel J. Shilatu
Ni miaka 55 imetimia
tangu jahazi lililowabeba Watanganyika na Wazanzibar liweke historia ya
kung’oa nanga mara baada ya Jamhuri Muungano wa Tanzania kuzaliwa rasmi
mnamo April 26,1964. Hii ilitokana na ujasiri, ushupavu na nia ya dhati
waliyokuwa nayo waasisi wa Muungano huu, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere (Tanganyika) na Abeid Aman Karume (Zanzibar).
Hatua hiyo ilifikiwa
kutokana na mtiririko wa kimazingira na mahusiano ambayo yalishabihiana
kama sio kufanana kabisa kwa pande zote mbili (Tanganyika na Zanzibar).
Zipo sababu za kijiografia, kisayansi, kitamaduni na kihistoria
zilizochangia huu muungano wetu.
Kutokana na sababu za
kijiografia na kisayansi inaaminika kabisa kwamba Visiwa vya Zanzibar
(Pemba na Unguja) vilikuwa vimeungana na hata kushikamana kwa pamoja
pembezoni mwa pwani ya ardhi ya Tanganyika. Hivyo tangu awali tulikuwa
ni kitu kimoja, tulio katika ardhi moja na ya pamoja.
Pia kuna historia
(isiyo na shaka) ya muingiliano wa kiutamaduni baina ya Wakazi wa
Tanganyika na Zanzibar ambapo hali nzima ya kuoa ama kuolewa ilizidi
kushamiri baina yao.
Halikadhalika
harakati za kudai ukombozi wa uhuru wetu ili tuweze kujitawala wenyewe
kutoka kwa dudu la wakoloni nazo zilichangia kutuunganisha. Inaaminika
(na ndiyo ilivyo) ya kuwa asilimia kubwa ya Wazanzibar walishiriki
kwenye harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Mwingereza
ambapo kutokana na nia, ushupavu na nguvu ya pamoja walifanikiwa kupata
Uhuru wa Tanganyika mnamo Desemba 9, 1961.
Lakini pia licha ya
asilimia kubwa ya Wazanzibar kushiriki katika mchakato wa Mapinduzi ya
Zanzibar lakini pia kulikuwepo na asilimia kubwa ya mchango wa ushiriki
kutoka kwa Watanganyika. Hatimaye matunda yake yalionekana ya mapinduzi
matukufu yaliyofikia kilele katika uwanja wa Gombani Pemba yaliyofanyika
Jamhuri 12, 1964, baada ya kuchoshwa na hila na ghiliba za Waarabu
uliotamalaki visiwani humo kwa zaidi ya karne mbili na hatimaye
waliwaacha wazalendo watwana katika ardhi yao.
Pia tusisahau lengo
na nia ya dhati aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere ya kutaka kuiunganisha
Afrika mzima kwa hatua lakini jitihada zake zilianza kuzaa matunda
ambayo hayatakaa yatokee tena Afrika kwa kuiunganisha Tanganyika na
Zanzibar.
Mnamo April 22, 1964,
Maraisi wa nchi hizi mbili ambazo sasa zinaunda Tanzania, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere (wa Jamhuri ya Tanganyika) na Abeid Amani
Karume (wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar ) walitia sahihi Mkataba wa
kimataifa wa kuunganisha nchi zao, unaojulikana kama “Hati ya Muungano”
(Articles of union) na hivyo kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar ama United Republic of Tanganyika and Zanzibar (URTZ) ambao ni
muungano sahihi kabisa kisheria na unaotambulika Kikatiba.
Siku ya Jumatatu ya
tarehe 26 Aprili, 1964 viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika
ukumbi wa Karimjee kwa nia ama lengo moja tu la kubadilishana “Hati za
Muungano”.
Wananchi wa Tanzania
walipiga kura kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa kwanza kabisa wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwaka 1965.
Kama nilivyodokeza
kwamba Muungano wa Tanzania ulifikiwa kwa kutiwa sahihi mkataba unaoitwa
Hati ya Muungano (Articles of the Union) na wakuu wa nchi hizi mbili,
Mwalimu Nyerere (Tanganyika) na Abeid Karume (Zanzibar) Aprili 22,1964
na kuridhiwa na mabunge ya nchi hizo Aprili 25, 1964 na hatimaye kuwa
sheria ya Muungano ya (Acts of Union) ya mwaka 1964.
Kimsingi sheria ya
Muungano ndiyo iliyoanzisha na ndiyo iliyopewa haki ya chombo cha
kikatiba kinachodhibiti katiba zote mbili za Serikali ya Muungano.
Mwanzoni kabisa Hati
ya Muungano (Articles of Union) iliyomo ndani ya sheria ya Muungano
iliorodhesha na hata kudadavua mambo 11 ya Muungano. Mambo hayo ni kama
vile:- Mambo ya nchi za nje, Ulinzi na usalama (lakini si usalama wa
Taifa); Polisi, Uraia, uhamiaji, mikopo na biashara za nchi za nje,
utumishi katika serikali ya Muungano, kodi ya mapato, usimamizi wa
fedha, Bandari, Usafiri wa anga, Posta na simu.
Kwa nia safi na
malengo mazuri yanayojitokeza Hati ya Muungano imekuwa ikiboreshwa zaidi
kwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele kwa malengo kusudi ya kuleta
umoja, mshikamano, amani na utulivu wetu ule ule tulioanza nao awali na
halikadhalika maridhiko yanayoendelea kuufanya Muungano huu uendelee
kudumu hadi hii kesho.
Ndio maana mtu
timamu hatoshangaa sana kuona Hati ya Muungano ikiendelea kuboreshwa
kila siku (na itaendelea hivyo) ambapo ilianzia na mambo 11 ambapo hii
leo yamefikia takribani 23.
Mengineyo ama baadhi
ya yale yalioongezeka ni kama vile;- Noti; Elimu ya juu,; Maliasili na
mafuta (mafuta) yasiyochujwa, bidhaa za mafuta na gesi asilia , ya mwaka
1968; Baraza la Mitihani ya Taifa; utafiti; utabiri wa hali ya hewa;
Takwimu,; Mahakama ya Rufaa ya juu ya mwaka 1979; pamoja na
uandikishwaji wa vyama vya kisiasa .
Tusisahau mwaka 1965
iliundwa katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (The Interim
Constitution of The United Republic of Tanzania) mpaka kufikia mwaka
1977 ndipo ilipoundwa katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambayo ndiyo inaendesha nchi hadi sasa.
Kukuru kakara za
Wazanzibari zinatookana na madai yao ya kuwa Tanganyika(Bara) imeimeza
Zanzibar (Visiwani) katika masuala mazima yahusuyo Muungano. Ikumbukwe
Ubaguzi wa dhana ya Tanganyika umeimeza Zanzibar si ya kweli na hii
imebainishwa katika katiba ya Muungano kuwa kuna Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Haya ni mapenzi ya
dhati waliyoonyesha kwa Wazanzibari kwa kuwaruhusu wawe na serikali yao
ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ikumbukwe Serikali ya Muungano inaongozwa na
katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inaongozwa na Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar na chombo chao
cha kutunga sheria kinaitwa Baraza la Wawakilishi.
Ndugu zangu hali ya
kupuuzia na hata kuuchezea Muungano wetu ni hatari sana tena ni dhambi
iliyotukuka. Mathalani Wazanzibari wakiamua kujiengua kwenye huu
Muungano ili wawe kivyao vyao,hawatabaki salama. Mwalimu Nyerere
alishawahi kusema ya kuwa “wakifika kwenye hatua hiyo watagundua kuwa
ndani yao kuna Wazanzibari na Wazanzibara”. Nao wataamua kuwafukuza wale
wa Wazanzibara, lakini hiyo haitakuwa mwisho. Punde si punde
watajigundua kuwa nao (Wazanzibari) wamegawanyika kwani kuna Wapemba na
Waunguja, na wakifikia hapo pia hawatakuwa salama ni lazima machafuko
yatatokea.
Daima Wazanzibari
watambue ya kuwa dhambi ya kutokutamalaki kwa dhana ya Unguja na Pemba
unatoka na kufunikwa na kivuli cha mwamvuli cha Muungano. Hivyo umoja,
mshikamano, amani na utulivu wao unategemea sana uwepo wa nguzo hii
imara ya Muungano huu tulionao.
Vivyo hivyo kwa watu
wa Bara (Tanganyika) ni rahisi kwao kutafunwa na dhambi ile ile ya
ubaguzi watakayo ianzisha nje ya uwepo wa Muungano ni rahisi sana kwa
ukabila, udini, ukanda na hata U-rangi kutamalaki ndani ya jamii
wakishafikia hapo, hawatabaki salama kwani watachafuana tu.
Muungano huu tulionao
unawafanya wale wageni, mataifa ya nje na watu wote wenye hila, donge,
roho ya korosho kuogopa kutugusa na kutuvuruga kutokana na kuwepo kwa
nguvu kubwa ya umoja, ushirikiano na mshikamano baina yetu.
Muungano huu wetu
unatupatia fursa kubwa ya uhuru wa kusafiri kwa pande zote iwe ni bara
ama ni visiwani. Leo hii ni rahisi sana kwa mtu wa bara kwenda Visiwani
na hata wale wa Visiwani kuja Bara kwa uhuru zaidi kwani Uhuru huo wa
uwepo wa nafasi hiyo umeshalipiwa na huu Muungano wetu tulionao.
Kutokana na uwepo wa
uhuru wa kusafiri usio na mipaka baina yetu, pia Muungano wetu tulionao
unazidi kutuongezea fursa na nafasi zaidi ya uwanja mpana wa ufanyaji
biashara. Hali hii imesababisha uwepo wa mzunguko mkubwa wa pesa ndani
yetu kwani si jambo la ajabu kuona pesa zikitoka Visiwani (Zanzibar)
kuja Bara (Tanganyika) kupitia mabadilishano ya bidhaa kama vile nafaka,
kahawa, matunda, vipuri vya magari na kadhalika.
Pia si jambo geni
tena kwa sasa kuona pesa zikivuka Bahari na kwenda visiwani Zanzibar kwa
ajili ya ufanyaji ama ununuzi wa biashara kama vile Magari, nazi,
Karafuu, Tende na kadhalika.
Muungano huu
unatuzidishia fursa ya mianya ya uwanja mpana tena usio na kikomo wa
ufanyaji biashara, Muungano huu hautubagui ama kutojulisha au kuwa na
upendeleo wa upatikanaji wa Elimu bora, huduma za kijamii bora, Muungano
hautugawi wala kuwa na upendeleo bali umejaa uwiano sahihi wa
upatikanaji wa mabo yote ya msingi yaliyomo ndani ya “Hati ya Muungano”
(Articles of union). Muungano huu ni nguzo imara katika muktadha mzima
wa nyanja za kimaisha yetu.
Ni ukweli uliodhahiri
kuwa haitakaa itokee Muungano kama huu (wa Tanganyika na Zanzibar) hapa
Barani Afrika umoja ushirikiano, ushikamano, amani na utulivu ni sehemu
mojawapo ya manufaa ya Muungano huu.
Njia mojawapo ya
kuwaenzi vyema waasisi wetu ni kwa kuudumisha Muungano wetu ambao ni
urithi wa aina yake waliotuachia. Watanzania yatupasa tuenzi Muungano
wetu kwa kuulinda na kuudumisha kwa vitendo kwani ni nguzo na fahari ya
kipekee na ya aina yake Barani Afrika.
No comments :
Post a Comment