Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine
Ndugulile akitoa hotuba yake kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa
Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali leo Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Afya Dkt.
Faustine Ndugulile akifuatilia mada ya kwanza ya Mkutano Mkuu wa Mwaka
wa Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali leo Jijini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu
wa Mwaka wa Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali wakifuatilia kwa
makini hotuba ya Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile leo
Jijini Dodoma.
……………………………..
Na Anthony Ishengoma
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema Serikali
haitazifumbia macho NGOs zote zinazojiingiza katika masuala
yanayohatarisha
usalama wa Nchi au kujiingiza katika vitendo visivyofaa
kama utakatishaji fedha na ugaidi.
Naibu Waziri Ndugulile amesema
hayo wakati wa hotuba yake alipokuwa akifungua Mkutano wa Mwaka wa
Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali uliondaliwa na Baraza la Taifa
la NGOs mapema leo Jijini Dodoma ambapo ameyataka Mashirika hayo kuepuka
vitendo vya udanganyifu.
Aidha Dkt. Ndugulile amewaambia
wajumbe wa Mkutano huo kuwa kuna baadhi ya NGOS ambazo zinafanya kazi
kwa udanganyifu bila kufuata malengo ambayo yamo katika katiba
zilizowasilishwa wakati wa usajili na badala yake zimejiingiza katika
matendo yanayohatarisha usalama na kuonya kuwa Serikali haitakuwa tayari
kuyapa nafasi Mashirika kama hayo kufanya kazi hapa Nchini.
Dkt. Ndugulile ameyataka Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali pia kuzingatii vipaumbele vya Taifa ili kuepukana
na changamoto ya mashirika mengi kufanya kazi katika eneo moja jambo
ambalo linaacha maswali kwa kuwa Tanzania ni moja kwa nini mashirika
mengi yanajielekeza na kutoa huduma sehemu fulani ya Nchi wakati kuna
maeneo mengine ya kipaumbele yanakuwa hayana mdau wa NGOs hata moja.
Aidha amezitaka NGOs zote Nchini
kuzingatia vipaumbele vya Serikali na kuacha tabia ya baadhi ya NGOs
zinazoitaka Serikali kufuata matakwa ya NGOs hizo katika suala zima la
mahali zinapotaka kufanya kazi.
Katika hotuba yake kwa Wajumbe wa
Mkutano huo Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa kwa sasa Serikali imekamilisha
kanzidata ya NGOs zote Nchini lakini pia kuweka mfumo wa kielektroniki
ili kuhakikisha taarifa zote za NGOS zinafika kwa wakati.
Aidha Naibu Waziri Ndugulile
amezitaka NGOs kote Nchini kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji
kama ambavyo NGOs zimekuwa zikiitaka Serikali kutekeleza wajibu huo na
kuziagiza kuhakikisha zinatangaza na kuweka wazi kiasi cha fedha
wanazopata kutoka kwa wafadhili wao ili jamii na Serikali wajue matumizi
ya fedha hizo lengo likiwa ni kushirikiana baina ya Serikali, wanufaika
na Mashirika hayo.
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Baraza la
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali unaendelea Jijini Dodoma ambapo Naibu
Waziri Ndugulile amewaambia Wajumbe wa Mkutano huo kuwa Serikali
inaendelea kuboresha Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
na kutumia fursa hiyo kuwambia wajumbe hao kuhusu kukamilika kwa uteuzi
wa Mwenyekiti wa Bodi ya Mshirika hayo Dkt. Richard Faustine Sambaiga.
No comments :
Post a Comment