Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na
wafanyakazi wapya (hawapo pichani) wakati wa mafunzo mafupi ya utendaji
kazi kwa wafanyakazi hao jana katika ukumbi wa taasisi hiyo Jijini Dar
es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Idara ya Rasilimali watu Bi. Ghati Chacha
Baadhi ya wafanyakazi wapya katika
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa
taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi (hayupo pichani) wakati wa mafunzo
mafupi ya utendaji kazi kwa wafanyakazi hao jana katika ukumbi wa
taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam. Jumla ya wafanyakazi wapya 22 ambao
ni wauguzi, mhandisi, afisa lishe na wataalamu wa dawa wameripoti tayari
kwa kuanza majukumu yao.
……………………..
Na: Genofeva Matemu – JKCI
Wafanyakazi wapya wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi
kwa bidii na kufuata
sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma kwa kutoa huduma bora na
maelekezo sahihi kwa wagonjwa.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) prof. Mohamed Janabi
wakati wa mafunzo mafupi ya utendaji kazi kwa wafanyakazi hao jana
katika ukumbi wa Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.
Prof. Janabi alisema kuwa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete ni kituo bora cha matibabu “center of excellence”
Afrika Mashariki na kati katika kutuo huduma za matibabu ya magonjwa ya
moyo hivyo ajira waliyoipata waitumie vizuri na kuleta tija katika nchi
ya Tanzania kwa kuepuka vitendo viovu vinavyoweza kuharibu majukumu yao
ya kazi.
“Nidhamu katika kutekeleza
majukumu ya kazi ni moja ya mafanikio ambayo mfanyakazi anaweza
kuyajenga kama atafanya kazi yake kwa utaratibu uliopangwa bila kuvunja
kanuni na sheria zilizopo” alisema Prof. Janabi
Aidha Prof. Janabi amewataka
wafanyakazi hao kuwahi kazini, kuwaona wagonjwa kwa wakati, kusoma na
kuelewa maelekezo kabla ya kutoa huduma kuipenda kazi yao pamoja na kuwa
na shauku ya kutaka kujifunza kutoka kwa wafanyakazi wengine
waliowazunguka.
Jumla ya wafanyakazi wapya 22
ambao ni wauguzi, mhandisi, afisa lishe na wataalamu wa dawa za binadamu
‘wafamasia’ wameripoti katika taasisi hiyo na kupata mafunzo mafupi
tayari kwa kuanza majukumu yao.
No comments :
Post a Comment