Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, akizungumza na viongozi
wa Serikali na watu wenye ulemavu wilayani Busega, wakati wa ziara yake
Wilayani humo Februari 27, 2019.
Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona, John
Daniel akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, wakati wa ziara yake
Wilayani humo Februari 27, 2019.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, akizungumza jambo na
viongozi wa Serikali na watu wenye ulemavu wilayani Busega, wakati wa
ziara yake Wilayani humo Februari 27, 2019.
Mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe.
Athony Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo
Kiswaga akizungumza na viongozi na watu wenye ulemavu wilayani Busega,
wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, Wilayani humo Februari 27,
2019.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera
akiwasilisha taarifa ya wilaya kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, wakati wa ziara yake
Wilayani humo Februari 27, 2019.
Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Watu
wenye ulemavu (SHIVYAWATA) Wilaya ya Busega, Makasi Egonjo akiwasilisha
taarifa ya watu wenye ulemavu kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, wakati wa ziara yake
Wilayani humo Februari 27, 2019.
…………………………….
Na Stella Kalinga, Simiyu
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
ametoa wito kwa wadau kuendelea kutoa msaada wa vifaa saidizi kwa watu
wenye ulemavu kwa kuwa hili ni hitaji endelevu kwa watu hao.
Mhe. Ikupa ameyasema hayo Februari 27,
2019 wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa
Serikali wilayani
Busega mkoani Simiyu wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani
humo.
Amewashukuru viongozi wa Wilaya ya
Busega kwa namna inavyowasaidia watu wenye ulemavu katika kuwapatia
vifaa saidizi huku akibainisha kuwa Serikali inaendelea kufanya jitihada
za kuwatafutia na kuwapatia watu wenye ulemavu vifaa hivyo kwa kadri
vitakavyopatikana.
“Napenda kuwashukuru viongozi wa Busega
kwa namna wanavyowasaidia watu wenye ulemavu kupata vifaa saidizi kama
fimbo nyeupe kwa wasioona, baiskeli na viungo bandia kwa walemavu wa
viungo, mafuta kwa wenye ualbino, lakini niwaombe wadau waendelee
kuwasaidia kwa kuwa hili ni hitaji endelevu katika kuishi kwao.” alisema
Mhe. Ikupa.
Katika hatua nyingine Mhe. Naibu Waziri
amesisitiza Kamati za watu wenye ulemavu kupewa miongozo ya namna ya
kuziendesha kamati hizo, ili ziweze kutimiza majukumu yake ipasavyo na
kuzitaka kutoa taarifa kuhusu fursa na masuala mbalimbali yanayowahusu
walemavu katika maeneo yao.
Vile vile Mhe. Ikupa amesema Serikali
inatarajia kuanzisha mfuko wa watu wenye ulemavu ambao utakuwa
ukishughulikia masuala mbalimbali ya watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja
na kutoa ruzuku kwa vyama vya walemavu.
Akitoa taarifa Mkuu wa Wilaya ya Busega,
Mhe. Tano Mwera, amesema Serikali wilayani imetoa baiskeli 17 kwa watu
wenye ulemavu wa viungo, zaidi ya fimbo nyeupe 50 kwa wasioona, mafuta
kwa watu wenye ualbino na Halmashauri imeandaa mpango maalum wa Mfuko wa
Bima ya Afya(CHF) iliyoboreshwa kwa ajili ya huduma za afya kwa
walemavu.
Kwa upande wao watu wenye ulemavu
wameiomba Serikali na wadau kuendelea kuwapa msaada wa vifaa saidizi ,
kupewa elimu ya kuunda vikundi na kuandaa maandiko ya miradi na kutoa
semina elekezi kwa kamati za watu wenye ulemavu.
“Mahitaji ya walemavu bado ni makubwa
tunaomba wadau mbalimbali waendelee kutukumbuka kutupa msaada wa vifaa
saidizi kama fimbo nyeupe kwa wasioona, viungo bandia na baiskeli kwa
walemavu wa viungo lakini na mafuta kwa wenzetu wenye ualbino” alisema
Katibu wa SHIVYAWATA Wilaya ya Busega, Makasi Egonjo.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutusaidia
kwenye mahitaji yetu mengi lakini tunaendelea kuomba wasichoke
kutusaidia, tunaomba maafisa ustawi wa jamii wawafikie watu wenye
ulemavu mpaka waliopo vijijini ili tuwe na elimu kuhusu mambo
yanayotuhusu na fursa za mikopo na ujasiriamali” alisema Mwenyekiti wa
Chama cha Wasioona, John Daniel
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Anthony Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo
Kiswaga amemhakikishia Naiba waziri Ikupa kuwa Mkoa wa Simiyu utaendelea
kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa katika ziara yake na
kuhakikisha walemavu wanashirikishwa na kufikiwa katika fursa
mbalimbali.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa amehitimisha ziara yake ya
siku tatu mkoani Simiyu Febrauari 27, 2019 ambapo alipata nafasi ya
kuzungumza na viongozi wa serikali, watu wenye ulemavu na kukagua mradi
wa kitalu nyumba katika Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu.
No comments :
Post a Comment