Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Binilith Mahenge akizungumza wakati mradi wa Lishe endelevu ukitambulishwa Dodoma
…………………………………………………………………….
Shirika
la Kimataifa la Kuhudumia Watoto la Save the Children kwa kushirikiana
na Delloite,Manoff na PANITA limetambulisha rasmi mradi wa lishe
endelevu kwa viongozi, watendaji na wadau wa maendeleo mkoa wa Dodoma
ili kuimarisha hali ya lishe kwa wanawake,vijana na watoto.
Uzinduzi
huo umefanyika leo Februari 28,2019 katika ukumbi wa Morena Hoteli
Jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa mkoa wa
Dodoma,Mheshimiwa Binilith Mahenge.
Mradi
huo wa Lishe Endelevu unalenga kuimarisha hali ya lishe kwa wanawake
walio katika umri wa kuzaa, wajawazito na wanaonyonyesha, vijana wa rika
la balehe na watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano ambao ni
waathirika wakubwa wa lishe duni.
Mahenge
alisema mradi wa Lishe Endelevu ni fursa kwa wananchi wa Dodoma hivyo
kuwaomba watendaji wa serikali kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wadau
wanaotekeleza mradi huo ili wafanye kazi katika mazingira ya amani na
utulivu kufikia malengo ya mradi.
“Malengo
ya mradi huu kimsingi yanaimarisha afya na lishe ya jamii ambayo ni
mtaji mkubwa katika kuimarisha nguvu kazi ya taifa haswa katika kipindi
hiki cha mpito kuelekea uchumi wa kati”,alieleza mkuu huyo wa mkoa.
“Tunawakaribisha
sana wadau wetu wa Lishe Endelevu na tuwatakia heri na mafanikio
makubwa katika utekelezaji wa malengo ya mradi. Twendeni tukiwa
tunakumbuka kuwa lishe bora ni msingi wa maendeleo ya Jamii, mkoa na
Taifa kwa ujumla, viongozi na watendaji wa mradi huu tekelezeni majukumu
yenu kama yalivyoainishwa kwenye malengo ya mradi”,alisema.
Katika
hatua nyingine alisema Lishe duni haiathiri tu maendeleo ya mtoto
lakini pia inaathiri ukuaji wake kimwili na kiakili kutoka kipindi cha
ujauzito na hatimaye kuathiri mchango wake katika maendeleo ya taifa kwa
kipindi chote cha uhai wake hivyo mradi huo utasaidia kuondokana na
changamoto hizo.
Aidha
aliwaomba wadau wa lishe mkoani Dodoma kuongeza jitihada kupunguza
utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano ingawa takwimu za hivi
karibuni (TDHS 2015/16) zimebaini kuwa Udumavu umepungua kutoka
asilimia 56.0 (2010) hadi asilimia 36.5 mkoani humo.
“Hali
ya lishe ya wanawake walio katika umri wa uzazi (miaka 15-49) nayo bado
ni mbaya; sote tunajua, hali ya lishe ya mama ikiwa mbaya inaathiri
hali ya mtoto toka tumboni pamoja na malezi na makuzi ya mtoto. Tafiti
za hivi karibuni zimebaini kwamba, kati ya wanawake kumi, wastani wa
wawili wana utapiamlo”,aliongeza.
Alibainisha
kuwa lishe duni kwa wanawake wajawazito inachochea hatari ya kujifungua
watoto njiti, waliodumaa au kuharibu mimba hivyo vifo vya wanawake
wajawazito vitapungua sana endapo serikali kwa kushirikiana na wadau
watakuwa na mikakati ya pamoja ya kutatua changamoto mbalimbali
zinazomkabili mama mjamzito, aliyejifungua na mtoto chini ya miaka
mitano.
Kwa
upande wake,Meneja wa Shirika la Save The Children mkoa wa Dodoma
Benety Malima aliwaomba wadau wa lishe mkoani humo na serikali
kushirikiana katika kutekeleza mradi huo ambao utasaidia kuimarisha hali
ya lishe kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa, wajawazito na
wanaonyonyesha, vijana wa rika la balehe na watoto walio na umri wa
chini ya miaka mitano.
Malima
alisema mradi huo unatekelezwa katika mikoa minne ya Dodoma, Rukwa,
Iringa na Morogoro kwa kipindi cha miaka minne Kwa miaka minne mradi
utagharimu USD 19.7 Milioni ukifadhiliwa na Mfuko wa Watu wa Marekani
‘USAID’.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkuu
wa mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Binilith Mahenge akitoa hotuba wakati
Shirika la Save the Children kwa kushirikiana na Delloite,Manoff na
PANITA likitambulisha mradi wa lishe endelevu kwa viongozi, watendaji na
wadau wa maendeleo mkoa wa Dodoma.
Mkuu wa mkoa wa Dodoma,
Mheshimiwa Binilith Mahenge akitoa hotuba wakati mradi wa lishe endelevu
ukitambulishwa kwa viongozi, watendaji na wadau wa maendeleo mkoa wa
Dodoma.
Meneja wa Shirika la Save The
Children mkoa wa Dodoma Benety Malima akiandika dondoo muhimu wakati
Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Binilith Mahenge akitoa hotuba wakati
mradi wa lishe endelevu ukitambulishwa kwa viongozi, watendaji na wadau
wa maendeleo mkoa wa Dodoma.
Viongozi, watendaji na wadau wa maendeleo mkoa wa Dodoma wakiwa ukumbini.
Picha ya pamoja viongozi, watendaji na wadau wa maendeleo mkoa wa Dodoma baada ya mradi mradi wa lishe endelevu kutambulisha.
No comments :
Post a Comment