Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa
Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro Bw. Mohamed Utaly, alipotembelea na
kukagua ukarabati wa Shule Kongwe ya Sekondari ya Wavulana ya Mzumbe.
Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akihoji baadhi ya maeneo ya
ukarabati wa Shule Kongwe ya Sekondari ya Wavulana Mzumbe, alipotembelea
na kukagua ukarabati wa Shule hiyo Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Mvomero
Mkoani Morogoro Bw. Florent Kyombo, akiiomba Serikali kushirikisha
uongozi wa Wilaya katika hatua za awali za utekelezaji wa miradi, wakati
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo
pichani) alipotembelea na kukagua ukarabati wa Shule Kongwe ya Sekondari
ya Mzumbe.
Mkuu wa Shule Kongwe ya
Wavulana ya Mzumbe Bw. Wal Kihongosi, akitoa maelezo ya maeneo
yaliyokarabatiwa huku wadau wengine wakitazama picha za majengo hayo,
wakati Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)
(hayupo pichani) alipotembelea na kukagua ukarabati wa Shule hiyo.
Mkuu wa Shule Kongwe ya
Wavulana ya Mzumbe Bw. Wal Kihongosi, akisoma kiasi cha fedha
kilichotengwa kwa ajili ya ukarabati wa Shule yake ambacho kilikua
kinatofautiana na kiasi alichowasilisha cha kutekeleza maboresho hayo.
Kushoto ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
(Mb).
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero
Mkoani Morogoro Bw. Mohamed Utaly, akiuliza jambo wakati Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kulia), alipotembelea
majiko ya Gesi yaliyo karabatiwa katika Shule Kongwe ya Wavulana Mzumbe,
Mkoani Morogoro .
Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa pili kulia), akiongozwa na Mkuu
wa Shule Kongwe ya Wavulana Mzumbe, Bw. Wal Kihongosi (kulia) kukagua
ukarabati wa shule yake.
Muonekano wamajengo ya Shule
Kongwe ya Wavulana ya Mzumbe, yaliyokarabatiwa na kubadilisha mandhari
ya shule hiyo yenye wanafunzi wenye vipaji.
(Picha na Peter Haule, Wizara ya Fedha na Mipango)
Na Peter Haule, WFM, Morogoro
Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amuagiza uongozi wa Wilaya ya Mvomero
mkoani Morogoro kuuchunguza mkataba wa ukarabati wa shule kongwe ya
Sekondari ya Wavulana-Mzumbe, ulioingiwa kati ya Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia na Shirika la Nyumba la Taifa-NHC ili kujiridhisha
kuhusu gharama halisi za mradi baada ya kubaini kiasi kinachodaiwa
kutumika kukarabati shule hiyo kinatofautiana na fedha halisi
zilizotolewa na Serikali
Dkt. Kijaji, ametoa maagizo hayo
alipotembelea na kufanya ukaguzi wa ukarabati wa shule kongwe ya
Sekondari ya wavulana ya Mzumbe iliyopo Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro
na kuelezwa na viongozi wa wilaya hiyo akiwemoo Mkuu wa Wilaya,
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kutokuwa na
taarifa zozote kuhusu mradi huo.
Dkt. Kijaji alishangazwa na
utofauti wa kiwango cha fedha kilichoainishwa katika taarifa ya gharama
ya ukarabati wa shule hiyo kwamba ilikuwa shilingi milioni 999.7 wakati
kiasi cha fedha kilichotolewa na Serikali ni zaidi ya shilingi bilioni
1.
Alitoa wito kwa wakuu wa wilaya
kote nchini kufuatilia kwa karibu miradi yote ya maendeleo
inayotekelezwa katika maeneo yao ili kujiridhisha kuhusu fedha
zinazotumika kwenye miradi hiyo, kukagua thamani ya fedha kwenye miadi
husika, pamoja na mikataba yote inayohusika ili kujua mawanda (scope) ya
miradi hiyo
“Kila anayekuja kutekeleza
miradi katika Wilaya ni vema akaulizwa amekuja kufanya nini na kwa namna
gani kwa kuwa lengo ni kuwasaidia wananchi wa maeneo husika na Taifa
kwa ujumla na hakuna siri kwenye miradi hiyo kwa hiyo ni lazima muijue
kwa undani” alisema Dkt. Kijaji
Alisema kuwa, Shule Kongwe ya
Mzumbe imekarabatiwa na mabadiliko yanaonekana lakini ni vigumu kujua
ilitakiwa kukarabatiwa kwa kiwango kipi na maeneo gani kwa kuwa wahusika
wakiwemo Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na Mkuu wa Shule hiyo hawafahamu
mawanda ya mradi huo.
“Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi
Mtendaji wa Wilaya ya Mvomero hakikisheni mnapata mkataba wa ukarabati
wa shule hii ili kupata uhakika wa nini kilitakiwa kifanyike kwa kuwa
bado maeneo mengi hayajakarabatiwa na Mkandarasi ambaye ni Shirika la
Nyumba la Taifa lakini tayari amekabidhi kazi” alisisitiza Dkt Kijaji.
“Dhamana ya Wizara ya Fedha na
Mipango ni kutafuta fedha, kupeleka maeneo husika kwa ajili kubadili
maisha ya watanzania na kukagua matumizi yake, hivyo hali hiyo
iliyojitokeza inaenda kufanyiwa kazi kwa lengo la kuongeza ushirikiano”,
alieleza Dkt. Kijaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Florent Kyombo,
aliishauri Serikali kuona namna bora ya kuboresha ushirikiano wakati wa
utekelezaji wa miradi kama hiyo kuanzia kwenye upembuzi yakinifu wa
majengo yanayokarabatiwa, nini kikarabatiwe, wakati gani, na kuwahusisha
wataalam wa wilaya wakati wa kukagua na kutathimini kazi iliyofanyika
kabla ya mkandarasi kulipwa
Naye Mkuu wa Shule hiyo Kongwe
ya Mzumbe Bw.Wal Kihongosi, aliishukuru Serikali kwa hatua yake ya
kuboresha shule hiyo ya vipaji maalum kwa kuwa hapo awali mazingira yake
yalikua hayasadifu hadhi ya kuwa na wanafunzi wenye vipaji.
Pia akaiomba Serikali kusaidia
kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi, kuongeza vifaa vya
maabara kwa kuwa havitoshi, kujengewa jengo moja jipya kwa ajili ya
ofisi ya taaluma pamoja na idara zake tisa na pia kuongeza idadi ya
watumishi wakiwemo wapishi na walinzi walioajiriwa wa muda mrefu badala
ya waliopo ambao ni wa mkataba wa mda mfupi ambao udhibiti wake
kulingana na unyeti wa kazi hizo ni mgumu.
No comments :
Post a Comment