Na; Mwandishi Wetu
Waziri wa Nishati Dkt. Medard
Kalemani amemtaka mkandarasi anayetekeleza kazi ya ujenzi wa Jengo la
Wizara ya Nishati linalojengwa katika Mji wa Serikali, Ihumwa jijini
Dodoma kuhakikisha kuwa anakamilisha kazi hiyo kwa wakati uliopangwa.
Akizungumza katika eneo la
Ihumwa Waziri Kalemani amesema kuwa, ili kufanikisha
utekelezaji wa
kazi hiyo kwa wakati ni vyema mkandarasi huyo ambaye ni Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) akahakikisha kuwa vifaa vyote vinavyotakiwa
katika kutekeleza kazi hiyo vinakuwepo katika eneo la kazi.
“Ni Lazima mkandarasi uhakikishe
kuwa matofali, mchanga, simenti, mabati, kokoto, rangi, madirisha,
nondo na vifaa vyote vinavyotakiwa hapa kwa ajili ya ujenzi
vinapatikana kwa wakati wote katika eneo hili la ujenzi ili kuharakisha
utekelezaji wa kazi hii kama ulivyopangwa na si vinginevyo”;
Akifafanua, Dkt. Kalemani
amesema kuwa atakuwa akitembelea eneo hilo mara kwa mara kuona hatua za
utekelezaji wa kazi hiyo na kuwaasa watendaji wa Wizara yake kuhakikisha
kuwa wanafuatilia kwa karibu kazi husika ili itekelezwe kwa viwango
vinavyotakiwa na kwa wakati.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo Dkt. Hamisi Mwinyimvua amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha
kuwa anaongeza mitambo inayotakiwa katika kutekeleza ujenzi huo ili
kuongeza kasi ya utekelezaji.
Ujenzi wa jengo la Wizara ya
Nishati ni utekelezaji wa Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa Wizara zote kujenga majengo katika
eneo hilo la Ihumwa unakojengwa mji wa Serikali unaojumuisha majengo ya
Wizara zote.
No comments :
Post a Comment