Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Maji Profesa, Makame
Mbarawa amevunja mikataba ya wakandarasi wawili waliokuwa na miradi
mikubwa ya maji katika mikoa ya Lindi na Kigoma na kusisitiza kuwa kamwe
hawawezi kufanya kazi na wakandarasi ambao ni madalali na wasio na
uwezo.
Pia amesema serikali kupitia wizara ya Maji imewekeza fedha
zaidi ya Sh.Trilioni 4.5 katika ujenzi wa miradi ya maji mijini na
vijijini.Profesa, Mbarawa,ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusubuvunjwaji wa mikataba ya ujenzi wa miradi ya Majisafi na Usafi wa Mazingira.
Aidha amesema kuwa miradi hiyo inayotekelezwa ipo mikubwa na midogo kwa kutumia fedha zao za ndani na mikopo ya masharti nafuu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Profesa Mbarawa aliwataja waliotimuliwa ni Overseas Infrastructure Alliance (India) Pvt Ltd aliyekuwa na mkataba wa kujenga mradi wa maji na usafi wa mazingira Mjini Lindi.
Mwingine ni Spencon Servise Ltd aliyekuwa anajenga mradi wa Maji Kigoma ambao wote kwa pamoja imeelezwa kuwa wamefirisika na hakuna uwezo tena.
Hata hivyo amesema kuwa katika hali ya kushangaza licha ya kuelezwa kuwa amefilisika lakini Overseas amerudishwa kuendelea na mradi wa maji wa Chalinze mkoani Pwani.
Waziri amesema kuwa kwa sasa makandarasi hao hawawezi kupewa miradi mingine mahali popote kwani wameitia serikali hasara kubwa na kuwapa usumbufu wananchi.
“Kwa sasa makandarasi wa hovyo wanaoharibu fedha za serikali haijalishi ni mzawa ama mzalendo lazima wamuondoe, nasisitiza kuwa mkandaras akifikisha chini ya asilimia 90 ni marufuku kupewa kazi nyingine,” amesema Mbarwa
Alifafanua kuwa Mkandarasi wa Lindi alipaswa kukamilisha mradi machi 2015 lakini tukamuongezea muda hadi desemba 2015 cha kushangaza hadi leo amefikia asilimia 92.3 tu akiwa amelipwa Sh, bilioni 27.925 kati Sh.bilioni 30.389.
Akizungumzia, Mkandarasi wa Kigoma amesema kuwa mkataba wake ulikuwa sawa na mwenzake lakini hadi sasa amefikia asilimia 87 akiwa amelipwa Sh Sh 39 bilioni kati ya 42 bilioni walizoingia mkataba na Wizara.
Kuhusu miradi hiyo amesema itaendelea kutekelezwa chini ya wakandarasi wengine ambao serikali itaingia nao mikataba.
Aidha Profesa, amesema kuvunjwa kwa mikataba hatakuwa na shida kwani wamejiridhisha maeneo yote kabla ya kufanya hivyo.
Aliwahakikishia wananchi kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kila mwananchi popote alipo anapata huduma ya majisafi na salama.
Hata hivyo amewataka wataalam hususan kitengo cha manunuzi kutowapatia kazi wakandarasi na wataalam washauri ambao tayari wana kazi wanazoendelea kuzikamilisha au zipo katika hatua za awali.
No comments :
Post a Comment