Opresheni ya kupambana na uvuvi
haramu katika ziwa Tanganyika kanda ya Kasanga, mkoani Rukwa imefanikiwa
kukusanya shilingi milioni 90 ndani ya mwezi mmoja ikiwa ni adhabu
mbalimbali kwa wavuvi waliokiuka sheria za uvuvi na.22 ya mwaka 2003
pamoja na sheria ya mazingira na.20 ya mwaka 2004.
Hayo yamesemwa na kiongozi wa
operesheni hiyo Geofrey Salaka wakati akitoa taarifa kwa mkuu wa mkoa wa
Rukwa Mh. Joachim Wangabo baada ya kutembelea katika soko la samaki la
kasanga na kuongea na maafisa wa operesheni hiyo.
Salaka alisema kuwa mbali na
kuwatoza faini hizo pia wamefanikiwa kutoa elimu na kuwahamasisha wavuvi
wadogowadogo kulipia leseni zao za uvuvi na leseni za vyombo
wanavyovitumia kwa shughuli za uvuvi kama sheria inavyotaka huku
akielezea changamoto wanazozipata katika kutekeleza majukumu hayo.
“Changamoto tunazozipata ni pamoja
na kukumbana na fujo kutoka kwa wananchi utoroshwaji wa samaki na mazao
ya uvuvi kwenda nje ya nchi, kuwepo raia wa kigeni wakijihusisha na
shughuli za uvuvi, hali ya hewa, upepo mkali, mvua na mawimbi ziwani,”
Alisema.
Kwa upande wake Mh. Wangabo
alipongeza juhudi hizo za kuhakikisha mapambano dhidi ya uvuvi haramu
hayarudi nyuma ili kutunza na kuhifadhi samaki na mazingira katika
ukanda wa Ziwa pamoja na Ziwa lenyewe na kusisitiza elimu iendelee
kutolewa kwa wavuvi ili washiriki katika kutunza mazingira.
“Tuendelee kuwaelewesha wavuvi,
vinginevyo wataendelea kuharibu rasilimali ya taifa letu, na hii ni
kwaajili yetu sisi na vizazi vinavyokuja, tukivua katika hali ambayo
haina uvuvi endelevu tutawafanya hawa samaki mwishoni watakwisha,
wakiisha hawa watu watakwenda wapi, maisha yao yanategemea hapa lakini
hawajui hilo, wanataka waharibu mpaka kambi sijui watalala wapi,”
Alisema.
Na kuongeza kuwa atahakikisha
anafanya mkutano na wananchi na wavuvi hao ili kuweza kuwaelimisha juu
ya madhara yanayoweza kujitokeza kama uvuvi haramu utaendelea
kutekelezwa bila ya usimamizi wowote.
Operesheni hiyo ilianza tarehe
19.10.2018 na Miongoni mwa zana zilizokamatwa katika operesheni hiyo ni
pamoja na Injini za boti 10, mitumbwi 48, magari 9 ya kusafirisha
samaki, pikipiki 4 zilizokuwa zinasafirisha samaki, samaki wachanga kilo
2050, nyavu 250 za makila chini ya nchi tatu pamoja na nyavu 20 za
timber (monofilament nets).
No comments :
Post a Comment