Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali, Bungeni jijini Dodoma, Novemba 15, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………….
Yazitaka mamlaka husika kudhibitiuingizwaji wa vyakula visivyokuwa na virutubisho
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
ameziagiza kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya kuhakikisha
zinachukua hatua kali dhidi ya watu wote watakaobainika wanaingiza
nchini bidhaa za chakula na mafuta ya kupikia kwa njia za magendo.
Kadhalika, Waziri Mkuu aziagiza
mamlaka husika kuhakikisha zinaendelea kudhibiti uingizwaji holela wa
bidhaa mbalimbali za vyakula visivyokuwa na virutubisho yakiwemo mafuta
ya kupikia na kutoa adhabu kali kwa wafanyabiashara watakaobainika
kuingiza bidhaa hizo nchini.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo
leo (Alhamisi, Novemba 15, 2018) wakati akijibu swali la mbunge wa Viti
Maalumu, Zainab Vullu katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa
Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma.
Mbunge huyo alihoji kuhusiana
na suala la uagizwaji wa mafuta ya kupikia kutoka nje kama unazingatia
sheria iliyopitishwa na Serikali ambayo inayolazimisha vyakula na mafuta
ya kula kuwekwa virutubisho.
Waziri Mkuu amesema ipo sheria
(Sheria ya chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219) inayohusu udhibiti wa
vyakula yakiwemo mafuta ya kupikia ambayo inasimamiwa na Mamlaka ya
Chakula na Dawa (TFDA) na imeweka utaratibu wa kudhibiti uzalishaji,
uagizaji, usambazaji pamoja na uhifadhi wa mafuta.
“Sheria hiyo pia inataka vyakula
vyote vikiwemo vile vilivyoagizwa kutoka nje ya nchi na vinavyozalishwa
hapa nchini yakiwemo mafuta ya kupikia, lazima viwekewe
virutubisho.Wafanyabiashara wanapaswa kuzingatia sheria na taratibu
zilizowekwa ili kulinda afya ya mlaji.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amesema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inakusudia
kuanzisha kurugenzi au idara itakayosimamia fukwe zote nchini zikiwemo
za bahari na maziwa ili kuziimarisha na kuzifanya ziwe miongoni mwa
vivutio vya utalii nchini.
Amesema kuimarishwa kwa fukwe hizo
kutawezesha watalii kupata maeneo ya kupumzika mara wanapotoka
kutembelea vivutio vingine vya utalii vilivyopo nchini kama mlima
Kilimanjaro pamoja na mbuga mbalimbali za wanyama.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati
akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Kiteto Zawadi Koshuma aliyetaka
kufahamu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukuza utalii nchini
kupitia fukwe zilizopo katika ukanda wa bahari na maziwa,
ambazo zimeachwa bila kuendelezwa.
No comments :
Post a Comment