Thursday, November 22, 2018

TPSF YADHAMIRIA KUENDELEA KUWEZESHA WAJASIRIAMALI NCHINI


Mratibu kutoka Taasisi ya Best Dialogue  Bi. Manka  Kway akizungumzia umuhimu wa Maktaba ya Mtandaoni inayoleta pamoja taarifa za wajasiriamali wa Tanzania ikiwemo tafifi mbalimbali zinazofanyika zikilenga kuchangia katika kukuza biashara hapa nchini.

Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka Taasisi ya Sekta  Binafsi (TPSF) Bw. Valency Mutakyamirwa  akizungumza na washiriki wa warsha ya siku mbili kuhusu uwezeshaji wa wanachama wa Taasisi hiyo leo Jijini Dodoma ikilenga kuibua changamoto na kuweka mikakati ya pamoja yakuzitatua.

Meneja Mradi kutoka Taasisi ya  Sekta  Binafsi  (TPSF)  Bi.  Veneranda   Sumila akisisitiza  kuhusu  umuhimu wa semina ya kuwajengea uwezo   wanachama  wa TPSF leo Jijini Dodoma wakati wa hafla yakufungua warsha hiyo.

Muwezeshaji  wa masuala ya Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Bw. Patrokil Kanje akizungumzia namna wajasiriamali wa Tanzania wanavyoweza kukuza na kuendeleza biashara zao  kwa kutumia mbinu za kisasa wakati wa warsha ya wanachama wa Taasisi ya Sekta Binafsi.

Katibu Mtendaji wa Umoja wa Wachimbaji wa Madini na Nishati  Tanzania (TCME) Bw. Gerald Mturi akizungumzia umuhimu wa semina hiyo kwa wanachama wa Taasisi ya Sekta Binafsi. (PICHA ZOTE NA MAELEZO)
NA MWANDISHI WETU 
TAASISI ya Sekta Binafsi Nchini imedhamiria kuendelea kuwajengea uwezo wajasiriamali nchini ili waweze kuzalisha na kukuza biashara zao na kuchangia katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. Akizungumza leo Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw. Valley Mutakyamirwa amesema kuwa  dhamira yao ni kuendelea kujenga uwezo kwa wajasiriamali hao  ili waweze kuchangika katika kutatua changamoto zinazowakabili  kwa kuweka mikakati ya pamoja kati ya wanachama wa Taasisi hiyo. “ Wajasiriamali hawa ni wanachama wetu hivyo jukumu letu ni kuhakikisha kuwa tunashirikiana nao katika kuibua changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ambayo tunashirikiana na Serikali katika kuona namna bora yakuzitatua “; Alisisistiza  Mutakyamirwa. Akifafanua amesema kuwa, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali ikiwemo kujenga miundombinu, kupunguza kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kutoka asilimia 20 hadi 18 hali inayoonesha dhamira ya dhati ya Serikali kuendelea kuimarisha mazingira ya wajasiriamali kufanya biashara. Aliongeza kuwa Warsha hiyo inawasaidia wajasiriamali hao kufanya tathmini ya shughuli wanazofanya na kuja na mikakati ya pamoja itakayoasaidia katika kuimarisha Biashara hapa nchini. Kwa upande wake Muwezeshaji  kutoka Taasisi ya Best Dialogue   Bi. Manka Kway  akizungumzia kuanzishwa kwa Maktaba ya Mtandaoni itakayokuwa na taarifa zote kuhusu masuala ya wajasiriamali zikiwemo tafiti, machapisho,fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo, Utalii, Biashara, Uwekezaji, Viwanda na miundombinu. Aliongeza kuwa kuwepo kwa maktaba hiyo kutasaidia kuimarisha na kusaidia kuinua kiwango cha Biashara hapa nchini kwa kuvutia wawekezaji na wajasiriamali wa ndani na nje ya nchi kuongeza uwekezaji na kuchochea maendeleo. Pia aliwataka wajasiriamali kutumia fursa ya kuwepo kwa  Maktaba hiyo kufuatilia taarifa mbalimbali zilizopo katika  maktaba hiyo ya mtandaoni katika kutafuta fursa mbalimbali zinazoweza kuimarisha utendaji wa wajasiriamali hao na kukuza sekta  husika. Katika maktaba hiyo ya mtandaoni wawekezaji kutoka katika mataifa mbalimbali wanaweza kupata taarifa zitakazowawezesha kuja kuwekeza hapa nchini  na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya Biashara na uwekezaji hapa nchini.Warsha ya kuwajengea uwezo wajasiriamali ambao ni wanachama wa Taasisi ya Sekta Binafsi inafanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma ikilenga kuwajengea uwezo wajasiriamali hao ili kuongeza tija kwa wajasiriamali hao hapa nchini

No comments :

Post a Comment