Thursday, November 22, 2018

RC GAMBO AANZA ZIARA YA SIKU TATU YA UKAGUA MIRADI MIKUBWA YA MAJI


 
Mkuu wa Mkoa wa Arusha akiangalia moja ya Visima ambavyo ni chanzo cha Maji yanayotarajiwa kuhudumia Jiji la Arusha.
Mkuu wa Mkoa Mrisho Gambo (wa kwanza kushoto) akipokea maelezo ya mapito ya mtandao wa maji taka.
Mafundi wa kampuni ya Cheil Engeneering wakiwa katika uchimbaji wa kisima kilichopo wilayani Arumeru
Miundo mbinu ya mfumo wa maji taka, mabwawa haya yanajengwa katika eneo la Terrat pembezoni mwa Jiji la Arusha. Mabwawa haya yanakadiriwa kuwa na uwezo wa kutibu takribani
Lita Milioni 22 kwa siku za Maji Taka.

Na. Vero Ignatus, Arusha 
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo ameanza ziara yake ya siku tatu katika wilaya za Arusha, Arumeru na Longido kukagua maendeleo ya Miradi Mikubwa ya Maji inayotekelezwa katika wilaya hizo.
Akiwa katika halmashauri ya Jiji la Arusha Gambo ametembelea mradi mkubwa wa Maji unaotekelezwa Jijini humo pamoja na baadhi ya kata za wilaya ya Arumeru.
Gambo ameitaka Bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafishaji Mazingira Jiji la Arusha AUWSA kuweka kipaumbele katika utunzaji wa vyanzo vya Maji vilivyopo katika mlima Meru ili kuhakikisha miradi hii inayotumia fedha nyingi inakua endelevu.
“Nimewahi kusikia wataalam wa Maji wakisema Vita ya Tatu ya dunia itahusisha kugombea maji, ninaomba sisi tuanze kujihami kwa kutunza vyanzo vyetu vya maji''alisema Gambo
Ameotaka bodi ya AUWSA kuandika andiko la mradi ambalo watalipigia debe katika Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia Mazingira ili kuweza kupata ufadhili wa kampeni hiyo ya utunzaji wa Vyanzo vya Maji. 
"Itakua haina maana kutumia kiasi kikubwa hivi cha fedha  ikiwa baada ya miaka michache ijayo vyanzo vyote vitakauka” alisema Gambo" 
Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) Mhandisi Ruth Koya alisema mradi huo utakamilika  Juni mwaka 2020 na wanatarajia Arusha itanufaika na mradi huo kwa kuwa ukosefu wa maji utakua historia.
"Kwa kuanza tayari wakandarasi wameanza kusambaza mtandao wa maji safi na taka kwa kuweka mabomba ya kisasa yanayoendana na mahitaji ya sasa, lengo ni mazingira yawe safi na wananchi wapate huduma za maji safi na taka kufikia asilimia 100 tofauti na hali ilivyo sasa ambapo ni asilimia 44 tu ya wananchi wanapata huduma hiyo,"alisema 
Amesema uzalishaji wa maji utaongezeka toka wastani wa lita Milioni 40 hadi lita Milioni 200 kwa siku na kushusha upotevu wa maji toka asilimia 40 za sasa hadi kufikia wastani wa asilimia 25.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya AUWSA, Dk.Richard Masika ameipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuweza kutoa fedha nyingi katika mradi huu mkubwa, pia ametoa rai kwa wananchi wa Arusha kuitunza miundo mbinu inayopita katika maeneo yao kwa ajili ya manufaa ya leo na baadae.
Mradi huu unatekelezwa kwa fedha za mkopo wa riba nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wa jumla ya shilingi zipatazo bilioni 520 (233.9 Mil. USD).
Gambo anaendelea na ziara yake katika wilaya ya Longido ambapo anatarajiwa kutembelea mradi wa Maji wa Mto Simba unaotarajiwa kumaliza kero ya Maji wilayani humo

No comments :

Post a Comment