Thursday, November 22, 2018

WAZIRI LUKUVI APIGA MARUFUKU HALMASHAURI NCHINI KUSHINIKIZWA KUPIMA VIWANJA NA WAMILIKI MASHAMBA


Waziri wa Ardhi Nyumba na Mendeleo ya Makazi William Lukuvi akifurahia jambo na mbunge wa jimbo la Babati Paulina Gekul (kulia) wakati wa ziara ya siku moja kutatua mgogoro wa ardhi  baina ya wananchi na wamiliki wa mashamba ya Singu na Endasago. Co Ltd.(Picha zote na Wizara ya Ardhi)

Waziri wa Ardhi Nyumba na Mendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi wa kijiji cha Singu wilaya ya Babati mkoani Manyara wakati wa ziara ya siku moja kutatua mgogoro  wa ardhi baina ya wananchi na wamiliki wa mashamba ya Singu na Endasago.

Wananchi wa vijiji vya Endasago na Dudiye vilivyopo wilaya ya Babati mkoa wa Manyara wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Mendeleo ya Makazi William Lukuvi wakati wa ziara ya siku moja kutatua mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na wamiliki wa mashamba ya Singu na Endasago.
Wananchi wa vijiji vya Endasago na Dudiye vilivyopo wilaya ya Babati mkoa wa Manyara wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Mendeleo ya Makazi William Lukuvi wakati wa ziara ya siku moja kutatua mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na wamiliki wa mashamba ya Singu na Endasago.

Mbunge wa jimbo la Babati Paulina Gekul akitoa shukuran kwa  Waziri wa Ardhi Nyumba na Mendeleo ya Makazi William Lukuvi kwa kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 30 baina ya wananchi wa Singu na Endasago na wamiliki wa mashamba ya Singu na Endasago.
NA MUNIR SHEMWETA, BABATI
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amepiga marufuku halmashauri zote nchini kupima viwanja kwa shinikizo la wamiliki wa mashamba makubwa na kusisitiza kuwa kazi hiyo inapaswa kufanywa na  halmashauri ambazo ndizo zenye jukumu la kupanga miji nchini.
akizungumza na wananchi wa kijiji cha Singu wilaya ya Babati mkoani Manyara Lukuvi alisema uamuzi wowote wa kupima viwanja unatakiwa kuratibiwa na halmashauri husika kwa kuzingatia mipango miji na si vinginevyo kwa kuwa mwenye  dhamana ya kupanga miji ni halmashauri.
Agizo la Waziri Lukuvi linafuatia kuelezwa na halmashauri za wilaya ya Babati kuhusu mpango wa kupima viwanja katika eneo la shamba la Singu Estate linalomilikiwa na kampuni ya Agric Evolution Ltd .
Lukuvi ameziagiza halmshauri za Mji na ile ya wilaya ya Babati kuainisha mipaka na kupima eneo la vijiji vya Singu, Sigino na Daglailoy vilivyopo kata ya Singu wilaya ya Babati sambamba na kuvipatia hati vijiji vyote na kubainisha kuwa zoezi la kugawa viwanja katika  shamba linalomilikiwa na kampuni ya Agric Evolution ltd litafanyika baadaye kwa utaratibu utakaopangwa.
Lukuvi alisema ameamua kusitisha ugawaji viwanja baada ya kubaini ukiukwaji wa taratibu sambamba na baadhi ya wawekezaji kununua mashamba katika maeneo ya mjini kwa nia ya kuzishawishi halmshauri kupima viwanja badala ya halmashauri kupima kulingana na mipango yake.
" kumekuwa na mtindo wamiliki wa mashamba wanachukua maeneo ambayo wanaona yanakaribia kuwa miji kwa lengo la kupima viwanja na kuwalambisha asali  watendaji wa halmashauri ili malengo yao yatimie" alisema Lukuvi.
Aidha, Waziri wa ardhi Nyumba na maendeleo ya makazi william Lukuvi ameagiza wananchi 14 waliojenga katika shamba la Endasago lililopo kata ya Ari wilaya ya Babati mkoa wa Manyara unapopita mradi mkubwa wa umeme Kilowat 400 kulipwa fidia na kuondoka eneo hilo.
Uamuzi wa kulipa fidia kwa wananchi hao unatoa suluhu ya muda mrefu baina ya mmiliki wa shamba kampuni ya Endasago co ltd na wananchi waliojenga katika njia ya kupitisha umeme wa mkongo kutoka Singida kupitia Babati, Namanga mpaka Kenya huku utata ukiwa ni nani anastahili kulipwa fidia kati ya pande hizo mbili.
Amelitaka shirika la Umeme tanesco kuendelea na zoezi la kuweka nguzo kwa ajili ya kukamilisha upitishaji nyaya za umeme katika mashamba yote mawili ya Endasago na Singu lakini malipo ya fidia yatakuwa kwa wale wananchi wa kijiji cha Endasago pekee.
"Tanesco muendelee na uwekaji nguzo katika mashamba yote mawili na wananchi wasimame kufanya shughuli yoyote wakati wa zoezi hilo.
Pamoja na uamuzi wa fidia, Lukuvi ameitaka halmashauri ya wilaya ya Babati kupima upya eneo la shamba la Endasago na kumpatia  mmiliki wake  eneo kulingana na mahitaji yake. Aidha, alimuagiza mmoja wa wana hisa wa Kampuni ya Endasago Abraham Mchinja kufuatilia hati ya shamba pamoja na kuhuisha umiliki wa kampuni ya Endasago co Ltd ambayo wanahisa wake wawili wamefariki dunia na kubaki mmoja pekee.
Mbunge wa jimbo la Babati Paulina Gekul aliiomba serikali kuangalia namna ya kuwasaidia wananchi wa vijiji vya Endasago na Singu dhidi ya wamiliki wa mashamba hayo mawili kwa kuwa wananchi wa vijiji hivyo wamekuwa wakiishi eneo hilo kwa muda.
Kwa muda mrefu kumekuwa na mgogoro mkubwa baina ya wananchi wa vijiji vya Singu, Sigino na Daglailoy vilivyopo kata ya Singu na vile vya Endasago na Dudiye vilivyopo kata ya Ari wilayani Babati na wamiliki wa mashamba ya Endasago lenye ukubwa wa  1300 na Singu ekari 3013 kuhusiana na umiliki wa mashamba.

No comments :

Post a Comment