Na Innocent Mungy
Serikali ya Tanzania imejikita
katika kuhakikisha kuwa Sekta ya TEHAMA inakuwa chachu ya kufikia kuwa
nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ili kutimiza malengo ya
millennia ya maendeleo endelevu kabla ya mwaka 2030.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibuu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Jim Yonazi jijini
Dubai unakofanyika Mkutano Mkuu wa Nchi wanachama wa Shitika la
Umoja
wa Mataifa linalosimamia Mawasiliano duniani (International
Telecommunication Union – ITU).
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaac Kamwelwe, Dkt. Yonazi
amesema Serikali imejizatiti kuhakikisha kuwa, uchumi wa Tanzania
unachangiwa kwa kiasi kikubwa na sekta ta TEHAMA.
“Napenda kutumia nafasi hii
kuiarifu dunia kupitia Mkutano huu maendeleo makubwa ya TEHAMA
yanayofanyika nchini Tanzania kupitia kupitia Serikali ya awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kufuatia
uchaguzi wa mwaka 2015, Serikali iliyoko madarakani hivi sasa
imetayarisha Sera Mpya ya TEHAMA inayoelekeza umuhimu wa TEHAMA katika
kujenga uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania”, alisema Dkt. Yonazi.
Aidha, Dkt. Yonazi alisema Sekta
ya TEHAMA imekuwa kwa kiwango kikubwa sana nchini na kubadilisha maisha
ya Watanzania walio wengi vijijini na mijini pia. Aliongeza kuwa
ushahidi wa maendeleo ya TEHAMA nchini unaonekana katika idadi ya watoa
huduma za TEHAMA nchini, matumizi ya teknolojia mbalimbali, idadi ya
watumiaji wa huduma mbalimbali zikiwamo za intaneti, simu na hata redio
na runinga katika mifumo mbalimbali kupitia TEHAMA.
Alisema, katika kukuza matumizi ya
TEHAMA, Tanzania imeamua kuruhusu teknolojia mbalimbali (technology
neutrality) na kuwekeza katika kujenga mkongo wa taifa katika
kuunganisha kila mkoa nchini. Kadhalika, mkongo huo umeunganishwa na
nchi jirani zilizopakana na Tanzania. Pia alizungumzia kuhusu Tanzania
kuwekeza katika kituo cha kutunza data cha kiwango cha kimataifa (Tier 3
data Centre).
Hali kadhalika Dkt Yonazi
aliuambia Mkutano huo kuwa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote,
Tanzania imeweza kuwa na watumiaji zaidi ya 41 milioni hadi kufikia juni
2018 ambayo ni sawa na kufikia 94% ya nchi nzima, huku wastani wa
watumiaji wa intaneti ikifikia 45% kati ya watanzania wapatao milioni
55. Alisema nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa maeneo
yaliyobaki yanafikiwa mwaka 2020.
Dkt. Yonazi alikumbushia Mkutano
huo kuwa, Tanzania ilikuwa moja ya nchi za mwanzo kabisa kuingia katika
mfumo wa utangazaji wa dijitali na hivyo kuruhusu masafa katika bandi
700 yaliyokuwa yanatumikakatika mfumo wa analojia na sasa yanatumika
katika mfumo wa intaneti wa mwendo kasi ili kuongeza chachu ya maendeleo
ya uchumi wa Tanzania kupitia TEHAMA.
“Kufuatika maendeleo makubwa ya
TEHAMA nchini, Tanzania inakaribisha wawekezaji katika sekta hii ili
kuweza kushirikiana na sisi katika kuboresha TEHAMA na maendeleo ya
wananchi wetu kwa ujumla” alisema DKt Yonazi alipokuwa nahitimisha
hotuba yake.
Tanzania inashiriki katika Mkutano
huu wa ‘ITU Plenipotentiary Conference’ unaofanyika mara moja kila
baada ya miaka 4 ambapo chaguzi mbalimbali zitafanyika kuchagua viongozi
wakuu wa ITU na nchi zitakazoingia katika Baraza la Utawala la ITU (ITU
Council) ambapo Tanzania inagombea kuwa miongoni mwa nchi 13 za Afrika
kuingia katika Baraza hilo. Katika uchaguzi uliofanyika leo Alhamisi
tarehe 1 Novemba, Katibu Mkuu Houlin Zao na Naibu Katibu Mkuu Malcolm
Johnson wamechaguliwa tna kuendelea na nyadhifa zao kwa miaka mingine
minne.
No comments :
Post a Comment