Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, akiwa katika picha ya pamoja na
wafanyabiashara wa mafuta wa Uganda mara baada ya kukutani nao jijini
Mwanza.
……………………………………………………………………………..
Serikali imewahakikishia
wafanyabiashara wa mafuta kutoka uganda kuwa imejipanga kutatua
changamoto zote zilizopo kwenye usafirishaji ili kupunguza gharama za
uchukuzi kati ya Tanzania na nchi hiyo.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, amesema hayo
wakati wa kikao
maalum kilichowakutanisha wafanyabiashara wa Mafuta wa Uganda na taasisi
za Uchukuzi za Tanzania na kusema kuwa Serikali inatekeleza hayo kwa
kuboresha miundombinu ili kuvutia wafanyabiashara wengi zaidi
“Niwahakikishie kuwa changamoto
zote zilizoainishwa baada ya majumuisho ya ziara yenu ya siku 5 nchini
tutazifanyia kazi”, amesema Naibu Waziri Nditiye.
Aidha, Naibu Waziri Nditiye
ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ikiwemo upanuzi
wa bandari,ukarabati wa reli na ukarabati wa meli ili mizigo
inayokwenda Uganda kupitia bandari ya Dar es Salaam ifike kwa wakati.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa
Kampuni ya Meli, Eric Hamis amesema mpaka sasa tayari wamesafirisha
zaidi ya tani elfu kumi na tano za Uganda kwa kutumia meli ya MV Umoja
na kusema kuwa wamejipanga kusafirisha mzigo mkubwa zaidi kabla ya mwaka
wa fedha kuisha.
Sisi kama Kampuni ya meli
tuliifanyia ukarabati meli ya MV Umoja na imekuwa ikisafirisha mzigo wa
Uganda na niwahakikishie kuwa kupitia ziara hii na jitihada nyingine
tunazozifanya tutapata wafanyabishara wengine ambao watasafirisha mizigo
yao kwa kutumia meli hii” amesema Hamis.
Kwa upande wake Mchumi Mwandamizi
kutoka Wizara ya Ujenzi ya Uganda, Gerald Akini, amemwahidi Naibu
Waziri Mhandisi Nditiye kuwa yale ya kisera yanayohusu Uganda
atayafikisha katika ngazi husika ili yafanyiwe kazi ili kuimarisha
ushirikiano uliopo kibiashara.
Bw Gerald ameishukuru Serikali ya
Tanzania kwa utayari wake wa kuwapokea wafanyabiashara na kuweka
mazingira mazuri ili watumie bandari ya Dar es Salaam.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa
kuendelea kuboresha miundombinu ikiwemo kupunguza vituo vya
mizani,ujenzi wa reli ya kisasa,uboreshaji wa bandari na kuahidi
kuendeleza ushirikiano kwa kushawishi wafanyabiashara wengi zaidi
kutumia bandari ya Dar es salaam.
Wafanyabiashara wa mafuta kutoka
nchini Uganda wamefanya ziara ya siku 5 nchini ambapo wametembelea
bandari ya Dar es salaam, Tanga,Mwanza pamoja na kukagua miundombinu ya
reli na meli za kampuni ya meli na kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa
na Tanzania kuimarisha biashara baina ya nchi hizo.
No comments :
Post a Comment