Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba wakati
alipowasili kwenye kiwanda cha Chai cha Mponde wilayani Lushoto
akiwa katika ziara ya Mkoa wa Tanga, Novemba 1, 2018. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akitazama mitambo ya kiwanda cha Chai cha Mponde wilayani Lushoto
Novemba 1, 2018. Kushoto kwake ni Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Charles Mwijage. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akitazama mitambo ya kiwanda cha Chai cha Mponde wilayani Lushoto akiwa
katika ziara ya Mkoa wa Tanga, Novemba 1, 2018. Alikuwa katika ziara ya
Mkoa wa Tanga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akikagua kiwanda cha Chai cha Mponde wilayani Lushoto, Novemba 1, 2018.
Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, watatu kulia ni Mkuu
wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela na wanne kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa
Mkoa wa Tanga, Henry Shekifu.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwapungia wananchi wa Mponde wilayani Lushoto wakati alipowasili
kijijini hapo kukagua kiwanda cha chai cha mponde na kuzungumza na
wananchi, Novemba 1, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiteta na Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba katika mkutano
aliouhutubia kwenye kijiji cha Mponde wilayani Lushoto, Novemba 1, 2018.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Wananchi wakimpungia Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa wakati alipowasili kwenye kijiji cha Mponde wilayani
Lushoto kukagua kiwanda cha chai cha Mponde na kuzungumza na wananchi,
Novemba 1, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwasalimia wananchi wa Bumbuli wilayani Lushoto akiwa katika ziara ya
Mkoa wa Tanga, Novemba 1, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwasalimia wananchi wa Bumbuli wilayani Lushoto akiwa katika ziara ya
Mkoa wa Tanga, Novemba 1, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………
*Yaagiza mashine zichunguzwe, mitambo yenye hitilafu ikarabatiwe kazi ianze
SERIKALI imemaliza mgogoro
uliodumu kwa miaka mingi kati ya wakulima wa chai wa
wilaya za Lushoto
na Korogwe na kampuni ya Mponde Tea Estate uliosababisha kufungwa kwa
kiwanda cha chai cha Mponde baada ya kuagiza kiwanda hicho kianze kazi.
“Waziri Mwijage na Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Kilomo Prof. Siza Tumbo hakikisheni kazi ya kukagua
kiwanda na mitambo inafanyika haraka na kubaini mitambo ipi ni mizima na
ipi ina hitilafu ili ukarabati ufanyike na kiwanda kianze kazi mara
moja.”
Uamuzi huo wa Serikali
umetangazwa leo (Alhamisi, Novemba 1, 2018) na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye kijiji cha Kweminyasa kata ya Mponde, wilayani
Lushoto baada ya kutembelea kiwanda hicho .
Waziri Mkuu amesema mwaka 1999
Serikali iliamua kuwapa wakulima wa chai na kiwanda hicho kwa ajili
kuwawezesha kuwa na sehemu ya kuchakata chai yao lengo likiwa ni
kuwajengea uwezo wa kiuchumi. Imeamua kukirudisha Serikali baada ya
kuwepo migogoro iliyoathiri uzalishaji kiwandani hapo.
Kuhusu suala la madeni ya
watumishi, ameagiza watafutwe na madai yaorodheshwe kwa ajili ya malipo,
amewahakikisha wananchi hao kuwa suala la ajira ambazo zilipotea baada
ya kiwanda kufungwa zitarudi kwa sababu Serikali inataka kuona kiwanda
kikifanya kazi.
“Serikali imeamua kukichukua
kiwanda hiki ambacho awali ilikikabidhi wakulima wa chai na kwamba
itahakikisha lengo lake la kuboresh kilimo linafanikiwa na wakulima
wanaendelea kulima zao la chai. Hatutaki kusikia masuala ya Utega wala
Mponde hapa si mahali pake.”
Amesema wakulima hao walikosea
kwa kuunda Umoja wa Wakulima wa Chai (UTEGA) ambapo katika kusajili
badala ya kuanzisha ushirika wao walisajili NGO ambayo ilikuwa na
wanachama wake, huku kiwanda kikiwa kimeanzishwa kwa ajili ya wakulima
wote, jambo ambalo lilisababisha mgogoro baina ya wakulima na viongozi
wa UTEGA.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa wakati
mgogoro huo ukiendelea kati ya UTEGA na wakulima wa chai wasiokuwa
wanachama wa NGO hiyo, uliibuka mgogoro mwingine baina ya wakulima wote
pamoja na muwekezaji ambaye ni kampuni ya Mponde Tea Estate baada ya
kukabidhiwa kiwanda hicho na uongozi wa UTEGA bila ya wao
kushirikishwa.
Amewasisitiza wakulima
wafufue mashamba yao kiwanda ni cha Serikali hivyo watakuwa wamepata
sehemu ya uhakikika ya kupeleka chai ambayo itachakatwa. Pia ameagiza
Mrajisi wa Ushirika aende kwa wakulima na kutambua idadi yao pamoja na
kujua ukubwa wa mashamba yao.
Amesema baada ya kubaini idadi ya
wakulima na ukubwa wa mashamba yao awasaidie katika kuunda vyama vya
ushirika vya msingi (AMCOS) kisha kuunda ushirikia wao ambao watautumia
katika kusimamia zao lao la chai na kuhakikisha mkulima ananufaika.
Waziri Mkuu amesema zao la chai
ni miongoni mwa mazao makuu sita ya kimkakati, mengine ni korosho,
kahawa, tumbaku, pamba na chikichi, hivyo amewataka wafufue mashamba yao
na waendelee kuiamini Serikali yao ambayo imejidhatiti kuwahudumia.
Awali,Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makam wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba alisma Mgogoro huo
wa kiwanda cha Mponde ulianza tangu mwaka 1999 na ilipofika mwezi Mei
2013, wananchi walimlalamikia kwa kushindwa kutatua tatizo hilo.
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa
Bumbuli aliwaomba wananchi hao waendelee kuwa na subira wakati suala lao
likiwa linaendelea kushughuliwa na Serikali. “Mgogoro huo umesababaisha
kudhorota kwa uchumi kwa sababu wananchi wengi waliacha kulima chai
baada ya kiwanda hicho kufungwa miaka mitano iliyopita.”
Hivyo Makamba ameiomba Serikali
iwasaidie wakulima wa zao la chai kuwapa miche mipya pamoja na pembe jeo
kwa ajili ya kufufua zao hilo na kukiwezesha kiwanda cha chai MPonde
kupata malighafi kama ilivyokuwa hapo awali.
Kwa upande wake, Waziri wa
Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema kuwa tayari
amekuja na wataalam kwa ajili ya kukagua mashine zote zilizopo kiwandani
hapo ili mchakato wa kukiwasha uanze mara moja.
Mwijage alisema “mimi kama Waziri
mwenye dhamana ya viwanda nawaambia wananchi muondoe wasiwasi tayari
kiwanda kimeshafunguliwa maana sitaondoka hapa Bumbuli mpaka kieleweke.”
No comments :
Post a Comment