Friday, November 30, 2018

SERIKALI YAAGIZA DORIA ZA MARA KWA MARA MAENEO YA MIPAKANI


Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa akikagua ukarabati wa Kituo cha Afya cha ushirombo wilayani Bukombe, Novemba 29, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa   akiweka Jiwe la Msingi la Ukarabati wa Kituo cha Afya cha Ushirombo wilayani Bukombe, Novemba 29, 2018. Kulia ni Mbunge wa Bukombe na Naibu waziri wa Madini, Doto Biteko na wapili kushoto ni  Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 Wanakwaya wa Ushirombo wakiimba wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipohutubia Mkutano wa hadhara kwenye Stendi ya Ushirombo, Novemba 29, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Bibi Mageni Simon akiwa mwenye furaha baada  ya kujifungua katika mazigira safi na salama ya  hospitali ya wilaya ya Geita ya Nzera iliyokaguliwa na kuzinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Novemba 28, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Lengo ni kudhibiti watu wanaoingia nchini bila ya kufuata taratibu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama kwenye maeneo ya mipakani kuendesha doria za mara kwa mara ili kuwabaini na kuwachukulia hatua watu wote wanaoingia nchini kinyemela bila ya kufuata taratibu.
“Suala la ulinzi na usalama ni muhimu, hivyo Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na viongozi wengine wahakikishe wanasimamia sheria na kuimarisha ulinzi hususan maeneo ya mipakani ili kudhibiti watu mbalimbali wanaoingia nchini kinyemela.”
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Novemba 29, 2018) alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Stendi ya Ushirombo wilayani Bukombe akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Geita.
Waziri Mkuu alisema ni muhimu kwa viongozi wa maeneo ya kuwa makini katika kufanya ukaguzi kwenye maeneo hayo ili wazuie uingiaji wa wageni kiholela kwa sababu baadhi yao si watu wema. “Serikali haizuii wageni kuingia nchini ila wafuate taratibu zilizowekwa.
Kadhalika, Waziri Mkuu aliwaagiza wakuu wa wilaya akiwemo na mkuu wa wilaya ya Bukombe, Said Nkumba watangaze fursa za uwekezaji zilizopo kwenye maeneo yao kwa lengo la kuvutia wawekezaji wa sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda ili kukuza uchumi.
Alisema viongozi hao wawasiliane na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kuwaeleza fursa za uwekezaji zinazopatikana katika maeneo yao, ambapo alitolea mfano wilaya ya Bukombe ambayo ina mifugo mingi, watafute wawekezaji wa kujenga kiwanda cha nyama.
Pia, Waziri Mkuu aliwashauri wafugaji nchini kufuga kisasa na kujiongezea tija, badala ya kutembeza mifugo kwa umbali mrefu wafuge kulingana na ukubwa wa maeneo yao ya malisho na marufuku kwenda kulisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima.
Mbali na kupiga marufuku wananchi kulisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima, pia Waziri Mkuu amezuia wafugaji kuingiza mifugo katika mapori ya akiba kwa kuwa mapori hayo kwa sasa yapo katika hatua za mwisho kutangazwa kuwa mbuga za Wanyama.

No comments :

Post a Comment