Friday, November 30, 2018

BILIONI 4 KULIPWA KILA SIKU KWA WAKULIMA WA KOROSHO-MHE HASUNGA


Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na waandishi wa habari   tarehe 29 Novemba 2018 katika Ukumbi wa Bodi ya Korosho Mjini Mtwara ili kutoa tathmini ya hatua zilizofikiwa na serikali za ununuzi wa korosho za wakulima.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na waandishi wa habari   tarehe 29 Novemba 2018 katika Ukumbi wa Bodi ya Korosho Mjini Mtwara ili kutoa tathmini ya hatua zilizofikiwa na serikali za ununuzi wa korosho za wakulima. (Picha Zote Na Mathias Canl, Wizara ya Kilimo)
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara
Serikali imetangaza kuongeza kasi ya malipo ya wakulima wa Korosho ili kufikia kiasi cha shilingi Bilioni nne (4) kila siku kwani kufanya hivyo zoezi la malipo kukamilika haraka.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 29 Novemba 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Bodi ya Korosho Mjini Mtwara ili kutoa tathmini ya hatua zilizofikiwa na serikali za ununuzi wa korosho za wakulima.
Amesema kuwa zoezi hilo litaenda sambamba na kuongezwa kwa wataalamu kwa ajili ya kuongeza nguvu ya malipo huku akisisitiza kuwa wataalamu wengine tayari wamekuwa na uzoefu wa namna ya kuhakiki na namna ya kulipa tangu kuanza kwa zoezi hilo.
Mhe Hasunga alisema kuwa mikoa inayolima korosho ni mingi nchini hivyo wakati tathmini sambamba na malipo zikiendelea timu ya wataalamu wengine itaundwa kwa ajili ya kuanza kufanya tathmini katika mkoa wa Pwani na mikoa mingine inayolima korosho nchini.
Katika hatua nyingine amesema kuwa serikali imejipanga kuwatambua wakulima wote wa korosho nchini ili kurahisisha kuwahudumia na kuainisha tathimini mahususi ya wakulima hao nchini.
Kuwafahamu wakulima hao itaisaidia serikali namna ya kushirikiana nao na kuwasaidia ili wakulima hao waweze kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo.
Miongoni mwa changamoto ilizokutana nazo serikali katika zoezi la uhakiki ni pamoja na kutotolewa takwimu sahihi na Vyama vya msingi vya ushirika za wakulima wa korosho kwani takwimu hizo zinatofautiana na vyama vikuu vya ushirika.
“Jambo hili la takwimu kwenda kinyume linatupa uhakika kwamba kuna taarifa zilikuwa zinapikwa ili kumnyonya mkulima lakini changamoto zingine ambazo zimetukumba ni pamoja na uchache wa maghala kwani yaliyopo hayatoshi” Alikaririwa Mhe Hasunga
“Kuna changamoto za mgomo wa wapakuaji na wapakiaji wa mizigo, nasi kama serikali tutakuwa na kikao hivi karibuni na wasafirishaji ili kuhakikisha kuwa wanalipwa fedha zao haraka iwezekanavyo baada ya kupitia mikataba yao kujiridhisha jinsi walivyokubaliana” Alisema
Tayari vyama 163 vya wakulima wa korosho vimekwisha hakikiwa mpaka kufikia jana jioni tarehe 28 Novemba 2018 kati ya vyama 617 vinavyojihusisha na zao la korosho nchini.
Katika vyama hivyo vilivyohakikiwa tayari malipo yamevifikia vyama 97 ambapo wakulima 22,269 wameshalipwa huku kiasi cha korosho ambazo zimekwishalipiwa ni kilo 6,712,681 huku jumla ya Bilioni 22,151,00,000.8 zikiwa zimekwishalipwa.
Aidha, mpaka kufikia jana jioni tarehe 29 Novemba 2018 serikali imekwisha hamisha kiasi cha Tani 9,347.2 kutoka kwenye maghala makuu.
Pia Waziri Hasunga ameyataja matarajio ya serikali katika uzalishaji wa Korosho kuwa ni takribani Tani 245,495.8

No comments :

Post a Comment