Thursday, November 15, 2018

Serikali Kuendelea Kupunguza Vifo Vya Watoto Wachanga Nchini


001
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza kwenye Kongamano la kwanza la kihistoria la Kisayansi la watoto njiti ambalo linafanyika Muhimbili kwa siku tatu kuanzia Novemba 15 hadi 17, 2018.
003
Rais wa Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania, Dkt. Sekela Mwakyusa akisisitiza jambo kwenye kongamano hilo leo kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Prof. Museru.
…………………
Serikali imesema inaendelea kuboresha maeneo ya kutolea huduma kwa watoto wa umri kuanzia sufuri hadi siku 28 wakiwamo watoto njiti katika hospitali za manispaa na wilaya nchini ili kupunguza vifo kwa watoto hao.
Hayo yamesemwa kwenye Kongamano la kwanza la kihistoria la Kisayansi la watoto njiti lililoanza leo tarehe Novemba 15 hadi 17, 2018 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambalo limewashirikisha wataalam wa watoto wachanga kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Akifungua Kongamano hilo kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru amesema Serikali imekuwa ikiratibu programu mbalimbali ili
kupunguza vifo vya watoto wachanga na wale wa chini ya miaka mitano.
Prof. Museru amesema asilimia kubwa ya watoto wa umri huo wanaozaliwa ni watoto njiti na kwamba takwimu zinaonyesha asilimia 13-17 ya watoto wote wanaozaliwa nchini Tanzania ni njiti.
“Tumeanza mipango wa kupunguza vifo vya watoto wachanga. Mipango hiyo ni kama kumsaidia mtoto kupumua baada ya kuzaliwa, kujenga wodi maalumu za watoto wachanga kwenye hospitali za manispaa na wilaya na kutoa mafunzo maalumu kwa wahudumu ili wajue namna bora zaidi ya kuwahudumia watoto wachanga.
Pia, Prof. Lawrence amesema katika kipindi cha miaka miwili Serikali kupitia wizara ya afya na TAMISEMI imehakikisha kunajengwa wodi za watoto wachanga katika hospitali zote nchini.
“Kwa kuanzia tulianza na huduma ya watoto njiti kwa mama kumkumbatia mtoto kifuani na sasa tumeanzisha wodi za watoto wachanga, tumeona mpango huu utasaidia  kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto za matibabu kwa watoto wachanga,” amesema  Prof. Museru.
Prof. Museru amesema lengo lingine la Serikali ni kuendelea kuwajengea kinamama mazingira mazuri ya kunyonyesha watoto na hivyo kufikia malengo ya kutoa huduma bora.
Naye Rais wa Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania, Dkt. Sekela Mwakyusa amesema moja ya changamoto katika kufikia malengo ya kutoa huduma bora kwa watoto hao ni ukosefu wa vifaa tiba na dawa maalumu ambazo humsaidia mtoto kupumua baada ya kuzaliwa.
Dkt. Mwakyusa amesema baadhi ya hospitali nchini zina vifaa tiba na dawa za kuwasaidia watoto kupumua baada ya kuzaliwa ikiwamo Hopitali ya Taifa Muhimbili.
“Malengo yetu ni kuboresha huduma kwa watoto wachanga, hivyo tayari tunatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wauguzi na madaktari jinsi ya kuwahudumia watoto hao.
Kongamano hilo litakuwa endelevu na litakuwa likifanyika kila mwaka katika kuadhimisha siku ya mtoto njiti (premature day)  duniani ambalo huadhimishwa Novemba 17, kila mwaka.
Kauli mbiu ya kongamano hilo ni ‘kila pumzi ni ya thamani’.

No comments :

Post a Comment