Na Grace Semfuko-MAELEZO.
Serikali kupitia Wizara ya Fedha
imesaini mikataba mitatu na Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB ya
kuipatia msaada na mikopo ya masharti nafuu yenye thamani ya dola za
Kimarekani 156.59 ambazo ni sawa na shilingi Bilioni 358.236 kwa ajili
ya
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mikataba hiyo ya Mikopo na Msaada
imesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Dotto James
na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB Dkt Alex Mubiru
ambapo kwa upande wa mikopo Serikali ya Tanzania itailipa kwa kwa muda
wa miaka 40 ijayo.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa
njia ya kusafirisha Umeme wa Msongo Mkubwa wa 400kV kuanzia Nyakanazi
Biharamuro Mkoani Kagera hadi Kigoma uliopata mkopo wa dola za
Kimarekani milioni 123.39, Mradi wa kudhibiti Sumu Kuvu kwenye mazao ya
nafaka ambao umepata dola milioni 33 zikiwepo dola milioni 20 za msaada
na dola milioni 13 za mkopo huku Bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/2019
nayo ikiongezewa mkopo wa masharti nafuu wa dola milioni 56 sawa na
shilingi Bilioni 128.28.
Akizungumza wakati wa utiaji saini
wa mikataba hiyo mitatu ya mikopo na msaada kati ya Tanzania na Benki
ya maendeleo ya Afrika AfDB, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango
Bw.Dotto James amesema Serikali itahakikisha miradi hiyo inatekelezwa
kama ilivyokusudiwa ili kuwaletea maendeleo Watanzania.
“Ndugu zangu hii ni hatua kubwa na
nzuri kwetu watanzania, hizi sio fedha ndogo, ni fedha nyingi ambazo ni
mkopo wa masharti nafuu pamoja na msaada kwenye eneo la kudhibiti Sumu
Kuvu za nafaka, tutalipa mikopo hii kwa muda wa miaka 40” alisema Dotto
James Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi
wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB Dkt Alex Mubiru amesema Benki hiyo
inalenga kuimarisha maendeleo ya Watanzania kwani fedha hizo zinaingia
moja kwa moja kwenye miradi ambayo itatumiwa na wananchi.
“Benki yetu ya Maendeleo ya Afrika
AfDB inalenga kuimarisha maendeleo ya wananchi, tuna miradi mingi
tunayofadhili kwa nchi za Afrika, kwa Tanzania pia tunayo miradi
tunayoimarisha, lengo la mikopo na misaada hii ni koboresha maishaya
watanzania” alisema Dkt Mubiru Mwakilishi Mkazi wa AfDB.
Zanzaibar ni miongoni mwa eneo
litakalonufaika na msaada huo kutoka Benki ya AfDB kwa upande wa
kudhibiti Sumukuvu kutoka kwenye mazao ya nafaka ambapo Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, Bw.Ahmad Kassim Haji amesema watahakikisha wanalinda
na kuhifadhi vizuri mazao yote ya nafaka na kwamba mradi huo
utawawezesha kufanya shughuli hiyo kikamilifu.
No comments :
Post a Comment