Moja ya eneo lililonufaika na mfumo wa majitaka ujulikanao kama
‘Simplified Sewerage’. Pichani ni Mtaa wa Unguja, Kata ya Mabatini Jijini
Mwanza ambao ni miongoni mwa maeneo yaliyonufaika na mradi wa majitaka wa
simplified sewerage kupitia ufadhili wa African Infrastructure Trust
Fund (EU-AITF).
Waziri
wa Maji Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) akikagua ubunifu uliotumika katika
ujenzi wa mradi wa majitaka, Mabatini mtaa wa Unguja wilaya ya Nyamagana. Mradi
huo umejengwa kwenye maeneo ya miinuko na umesaidia kuondosha uchavuzi wa
mazingira na magonjwa ikiwamo Kipindupindu.
Mkurugenzi
wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi
Anthony Sanga (mbele) akiwaongoza wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya
Maji Mjini Moshi (MUWSA) eneo la Mabatini Jijini Mwanza walipotembelea
kujifunza mfumo wa majitaka Oktoba, 2018. Ni mradi wa kipekee kuwahi
kutekelezwa nchini.
Mradi wa Majitaka unaotekelezwa kwenye maeneo ya miinuko Jijini
Mwanza unaofahamika kama "Simplified Sewerage" umekuwa miongoni mwa
miradi miwili bora zaidi kuwahi kutekelezwa Barani Afrika chini ya
ufadhili wa African Infrastructure Trust Fund (EU-AITF).
Hayo yameelezwa mwishoni mwa Mwezi Novemba, 2018 wakati wa
Mkutano wa kujadili miradi inayofadhiliwa na Benki ya Uwekezaji ya
Ulaya (EIB) kupitia mfuko huo wa EU-AITF.
Katika mkutano huo ilielezwa kwamba tangu mfuko huo uanzishwe
mnamo mwaka 2007 ni miradi miwili pekee ambayo imefuzu na kuwa miradi bora
zaidi kuwahi kutekelezwa ambayo ni Mradi wa Majitaka wa Simplified Sewerage wa
Jijini Mwanza, nchini Tanzania na mwingine ni mradi wa Nishati ya Umeme wa
Benin & Togo.
Akizungumzia mradi wa Majitaka wa Jijini Mwanza, Mshauri
wa masuala ya Kiufundi wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya, Raoul Pedrazzani
alielezea hali ilivyokuwa hapo awali kabla ya kujengwa kwa mradi mpya wa
majitaka kwenye maeneo ya milimani jijini humo.
Pedrazzani alisema kuwa kijiografia maeneo
mengi ya Jiji la Mwanza ni milima/miinuko na kabla ya mradi huo wa majitaka
wakaazi wa maeneo ya milimani hawakuwa na mfumo mzuri wa uondoaji wa majitaka
hali ambayo iliwasababishia adha mbalimbali ikiwemo uchafuzi wa mazingira na
maradhi.
Alisema suluhisho ilikuwa ni kubuni mradi
ambao utarahisisha utoaji wa majitaka kutoka kwenye makazi hayo kwenda
yanakostahili.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi
Anthony Sanga alithibitisha kupokea ujumbe wa pongezi juu ya ushindi huo.
Mhandisi Sanga aliipongeza Bodi ya
Wakurugenzi ya MWAUWASA kwa usimamizi mahiri wa shughuli zinazotekelezwa na
Mamlaka na pia aliwapongeza watumishi wote wa MWAUWASA kwa utekelezaji na
usimamizi mzuri wa miradi husika. “Mungu ni Mwema, tunamuomba Aendelee
kutusaidia. Hakika kwa pamoja tunaweza,” alisema Mhandisi Sanga.
Aliongeza kuwa lengo la Serikali ni
kuhakikisha huduma ya majitaka inapanuka zaidi ili wananchi walio wengi waweze
kufikiwa.
Maeneo ya miinuko ambayo tayari yamefikiwa na mfumo huo wa Simplified Sewerage ni Kilimahewa, Mabatini na Igogo na huku lengo likiwa ni kupanua wigo na kufikia maeneo mengi zaidi
No comments :
Post a Comment