Mbunge wa Buchosa Mkoani Mwanza Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Kulia) akifurahi jambo pamoja na Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo tarehe 22 Novemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo).
Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya kilimo wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo tarehe 22 Novemba 2018.
Picha ya pamoja waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb), Mbunge wa Buchosa Mkoani Mwanza Mhe
Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Naibu mawaziri wizara ya kilimo Mhe Omary
Mgumba na Mhe Innocent Bashungwa, na Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo
Mhandisi Mathew Mtigumwe wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi
wote wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo tarehe 22 Novemba 2018.
Mbunge wa Buchosa Mkoani Mwanza Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo tarehe 22 Novemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo).
Na Mathias Canal,
Wizara ya Kilimo-Dodoma
Aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba ambaye
ni Mbunge wa Buchosa Mkoani Mwanza leo tarehe 22 Novemba 2018 amemkabidhi rasmi
ofisi Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb).
Makabidhiano hayo yamefanyika katika Ukumbi wa mikutano
maarufu kama Kilimo IV Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Naibu mawaziri wa Kilimo
Mhe Omary Mgumba na Mhe Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo
Mhandisi Mathew Mtigumwe, na Wakuu wa idara na Vitengo.
Akizungumza katika hafla hiyo fupi Mhe Dkt Tizeba amempongeza
Mhe Hasunga kwa kuteuliwa kuhudumu katika nafasi hiyo ambapo amesisitiza kusimamiwa
kwa weledi huduma za ugani ambazo kwa kiasi kikubwa hakuna jambo la kujivunia
katika eneo hilo kutokana na mgawanyo wa kimajukumu kuwa katika wizara mbili ya
kilimo na TAMISEM jambo ambalo linapunguza ufanisi wa kiweledi.
Alisema kuwa wizara inapaswa kuendelea kusomesha wataalamu
mbalimbali nchini wakiwemo wa ugunduzi na utafiti ili kuongeza tija ya kilimo
na utoaji elimu kwa wakulima na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa wananchi
sambamba na Taifa kwa ujumla.
Vilevile amesema kuwa Wizara ya kilimo ni tanuru muhimu kwa
mahitaji ya wananchi hivyo inapaswa kutazamwa kwa karibu zaidi na serikali
ikiwa ni pamoja na kupewa fedha kwa wakati ili kukamilisha miradi mbalimbali
ambayo tayari imeanzishwa.
Kuhusu mfumo wa uzalishaji wa mbegu alisema kuwa serikali ina
Wakala wa mbegu za kilimo (ASA) ambao wanafanya kazi nzuri ya uzalishaji wa
mbegu lakini wanapaswa kuwezeshwa ili waweze kuzalisha mbegu kwa kutumia mfumo
wa umwagiliaji badala ya kuzalisha mbegu wakati msimu wa kilimo unaendelea.
“ASA wanazalisha mbegu wakati ambapo msimu wa kilimo umefika
hivyo mbegu zao zinakosa umuhimu kwa wakulima, hivyo wanapaswa kuzalisha mbegu kabla
ya msimu wa kilimo kufika” Alisisitiza Dkt Tizeba
Kuhusu mradi wa ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa unaendelea
vyema lakini hausimamiwi ipasavyo na Taasisi zingine za serikali zilizopewa
jukumu kubwa na muhimu la kusimamia shughuli hiyo wakiwemo Wakala wa majengo
Tanzania (TBA).
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)
amempongeza waziri huyo mstaafu Mhe Dkt Charles Tizeba ambaye ni Mbunge wa
Buchosa kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye wizara ya kilimo ikiwa ni pamoja na kusimamia
kwa weledi ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kipindi cha robo mwaka ya kwanza ya mwaka
2018/2019 ambayo imekuwa kwa asilimia 7.1
Waziri Hasunga alisema kuwa Dkt Tizeba ni mfano wa kiongozi
bora nchini ambaye ametekeleza majukumu yake kwa weledi na kutoa ushirikiano
mkubwa kwa viongozi wengine jambo ambalo linatoa chachu na kuonyesha jinsi
alivyo mzalendo kwa Taifa.
“Kutokana na alama alizoziacha Dkt Tizeba kwenye wizara ya
kilimo hakika tunastahili kumuona kama Mtakatifu kwani kulikuwa na changamoto
kubwa ya upatikanaji wa chakula nchini lakini alisimamia kidete na kuhakikisha
kuwa swala hilo linamalizika na sasa nchi ina ziada kubwa ya chakula hakuna
njaa” Alikaririwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa
“Dkt Tizeba alihakikisha kero ya Tozo na Kodi zinafutwa na kusaliwa
na Tozo na Kodi chache jambo ambalo limeongeza ufanisi katika wizara, usimamizi
huu mzuri uliofanywa hauwezi kusahaulika daima”
Mhe Hasunga aliongeza kuwa mfumo wa uagizaji mbolea wa pamoja
ulisimamiwa vizuri na Dkt Tizeba jambo hilo litasalia kuwa muhimu na alama kwa
Taifa.
Aidha, Alisema kuwa katika uongozi wa Dkt Tizeba nchi imezidi
kuimarika kupitia manufaa wanayoyapata wananchi kupitia mfumo wa stakabadhi
ghalani sambamba na mfumo wa ushirika ambao wananchi walipoteza imani kwa kiasi
kikubwa na Ushirika lakini kwa kipindi cha muda mfupi umeimarika kwa kiasi
kikubwa.
No comments :
Post a Comment