Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa wakati
alipowasili kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es salaam kufungua Mkutano wa
Baraza la Mawaziri la Nchi za Bonde la Mto Nile za Ukanda wa Maziwa
Makuu kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es salaam Novemba 22, 2018.
NA OWM, DAR ES SALAAM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaamesema
Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi za Ukanda wa
Maziwa Makuu katika kusimamia matumizi endelevu ya maji ya Mto Nile kwa
ustawi wa kiuchumi wa nchi zote. Ameyasema
hayo leo (Alhamisi, Novemba 22, 2018) wakati akifungua mkutano wa 21 wa
Baraza la Mawaziri la Nchi za Bonde la Mto Nile zilizopo Ukanda wa
Maziwa Makuu uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Rais Dkt.
John Magufuli. Amesema
nchi wanachama hazina budi kuimarisha ushirikiano ili ziweze kusimamia
vizuri matumizi endelevu ya maji ya Mto Nile pamoja na kushughulikia
changamoto zinazolikabili Bonde la Mto Nile. Waziri
Mkuu ametaja baadhi ya changamoto zinazolikabili Bonde la Mto Nile kuwa
ni pamoja na kushindwa kufikia makubaliano ya kuanzisha Kamisheni ya
Kudumu ya Bonde la Mto Nile. “Kwa takribani miaka 10 sasa tumeshindwa
kufikia makubaliano.”
Amesema,
sambamba na changamoto hiyo nchi wanachama zimekuwa zikichelewa sana
kutoa michango yao ili kuziwezesha taasisi zao kutekeleza ipasavyo
majukumu yao, jambo ambalo si tu linachelewesha maendeleo bali
linatishia usalama wa maji katika Bonde la Mto Nile.
Kufuatia
hali hiyo, Waziri Mkuu ametoa mapendekezo mbalimbali ili kuhakikisha
kunakuwa na matumizi endelevu ya rasilimali za maji kwenye Bonde la Mto
Nile pamoja na kusaidia nchi wanachama kupata maendeleo.
Moja
ya mapendekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu ni pamoja na nchi wanachama
kutoa elimu kwa wananchi wake kuhusu matumizi sahihi ya maji na umuhimu
wa kutunza vyanzo vyake ili kuhakikisha kunakuwepo na matumizi endelevu
ya maji.
“Suala
jingine ni ulipaji wa michango. Taasisi zetu haziwezi kutekeleza
majukumu yake kama hatulipi michango tena kwa wakati maana miradi ya
maendeleo haiwezi kutekelezwa kwa haraka kwa kutegemea wafadhili. Ni
vema nchi zikalipa michango.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema maji ni rasilimali muhimu duniani kwa ajili ya uhai
wa binadamu, maendeleo ya kiuchumi na kijamii hususani katika kuendesha
shughuli za kilimo, uvuvi, ufugaji, utalii na ujenzi, hivyo lazima
vyanzo vitunzwe.
Amesema
Bara la Afrika ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na matatizo
makubwa ya maji duniani, ambapo takwimu zinaonesha kuwa takribani nchi
14 hivi sasa zinakabiliwa na uhaba ama upungufu wa maji huku zingine 11
zinatarajiwa kuingia katika kundi hilo ifikapo 2025.
Waziri
Mkuu amesema kutokana na hali hiyo mikakati ya makusudi inahitajika ili
kuhakikisha chanzo hiko cha maji kinalindwa na rasilimali ya maji
katika Bonde la Mto Nile inatumika vizuri.
Mkutano
huo umehudhuriwa na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa ambaye ndiye
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Nchi za Bonde la Mto Nile zilizopo
kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Balozi Augustine Mahiga, Waziri wa Nishati Dkt. Medard
Kalemani.
Wengine
ni Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Awesu, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi
zao nchini, watendaji wa Sekretarieti ya Bonde la Mto Nile kutoka Ukanda
wa Maziwa Makuu pamoja na Ukanda wa Mashariki na maafisa wengine wa
Serikali.
Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Bw. George Lugomela (kulia) kuhusu mashine
ya kutambua uwepo wa maji ardhini kabla ya kufungua Mkutano wa
Baraza la Mawaziri la Nchi za Bonde la Mto Nile za Ukanda wa Maziwa Makuu
kwenye hoteli ya Serena, Novemba 22, 2018.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama burudani ya ngoma wakati alipowasili
kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es salaam kufungua Mkutano wa Baraza la
Mawaziri la Nchi za Bonde la Mto Nile za Ukanda wa Maziwa Makuu,
Novemba 22, 2018. Wapili kulia ni Waziri wa Maji, Profesa Mbarawa Makame na
watatu kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya
Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu)
No comments :
Post a Comment