Mhandisi Mshauri kutoka kampuni
ya Nicholas O’Dwyer Martin Hussey akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi
Joseph Nyamhanga (katikati), kuhusu hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa
barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port yenye urefu wa KM 112 kwa
kiwango cha lami, mkoani Rukwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga
(mwenye suti), akitoka kukagua daraja la Kalambo lenye urefu wa mita 84
lililopo katika barabara ya ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port yenye urefu
wa KM 112 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Rukwa.
Muonekano wa sehemu ya barabara
ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port yenye urefu wa KM 112 inayojengwa kwa
kiwango cha lami, mkoani Rukwa. Mradi wa ujenzi huo umekamilika kwa
asilimia 80.
Muonekano wa daraja la Kalambo
lenye urefu wa mita 84 ambapo ujenzi wake umekamilika. Daraja hilo lipo
katika mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya
Sumbawanga-Matai-Kasanga Port yenye urefu wa KM 112.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga
(mwenye suti), akikagua majengo yaliyobomolewa kupisha uboreshwaji wa
Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga, Mkoani Rukwa. Kushoto ni Kaimu Meneja
wa kiwanja hicho, Lucas Karoli na nyuma ni Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS) mkoni humo, Mhandisi Masuka Mkina.
Muonekano wa jengo la abiria
katika Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga ambapo hivi karibuni Serikali
itaboresha kiwanja hicho na utahusisha ujenzi wa jengo jipya la abiria,
ujenzi wa njia za kuruka na kutua ndege maegesho ya ndege, jengo la
kuongozea ndege, taa za kuongozea ndege na kituo cha hali ya hewa.
…………………………………………………………………
Serikali imetoa muda wa miezi
mitatu kwa mkandarasi anayejenga kwa kiwango cha lami barabara ya
Sumbawanga-Matai-Kasanga Port yenye urefu wa KM 112 kukamilisha ujenzi
huo.
Agizo hilo limetolewa mkoani
Rukwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta
ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, mara baada ya kukagua mradi wa
ujenzi wa barabara hiyo na kumtaka kuongeza kasi ya ujenzi huo.
“Hakikisheni mnaongeza kasi ya
ujenzi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili muikabidhi barabara hii
kwani imechukuwa muda mrefu”, amesisitiza Mhandisi Nyamhanga.
Amesema ujenzi wa barabara hiyo
inayojengwa na kampuni ya China Railway 15 group ni muhimu katika kuinua
uchumi ya nchi yetu katika sekta ya usafirishaji wa mizigo kupitia
bandari ya Kasanga kwani inaunganisha nchi yetu na nchi tatu ambazo ni
Burundi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia Ziwa
Tanganyika
Ameongeza kuwa mkandarasi mpaka sasa ameshalipwa madeni yake ya nyuma na hivyo hana sababu ya kutokuikamilisha barabara hiyo.
Aidha, Mhandisi Nyamhanga
amezitaja barabara ambazo zimekamilika ujenzi wake kwa kiwango cha lami
kuwa ni barabara ya Sumbawanga-Tunduma KM 225, barabara ya Sumbawanga –
Kibaoni KM 151 na barabara ya kutoka Sitalike hadi Sumbawanga Mjini KM
36.5
Amesema kuwa katika kuhakikisha
nchi yetu inaungana na nchi jirani, Serikali inaendeelea kutafuta fedha
kwa ajili ya barabara ya Matai hadi Kashesa yenye urefu wa KM 50
inayatuunganisha na nchi ya Zambia
Naye Meneja wa Wakala wa barabara
(TANROADS), Mhandisi Masuka Mkina, amesema mradi huo unagharimu kiasi
cha zaidi ya shilingi bilioni 133 na mpaka sasa mradi huo umekamilika
kwa asilimia 80.
Mhandisi Mkina amefafanua kuwa
mradi huo umehusisha ujenzi wa daraja kubwa la Kalambo lenye urefu wa
mita 84 ambapo limekamilika na KM 75 za barabara hiyo tayari
zimeshawekwa lami na kazi zingine zinaendelea.
Katika hatua nyingine Mhandisi
Nyamhanga amekagua Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga ambapo Serikali
imeshakamilisha maandalizi ya kuanza uboreshwaji wa kiwanja hicho na
tayari mkataba umeshasainiwa kati ya mkandarasi na Tanroads.
Ameagiza makampuni ya simu
yaliyojenga minara iliyopo karibu na uwanja huo kuondoa haraka ili
kutokwamisha mradi huo kukamilika mapema.
Amesema kuwa Serikali imetoa
bilion 3.7 kwa ajili ya fidia na wananchi wameonesha ushirikiano kwa
kubomoa majengo yao hivyo ujenzi hauna vikwazo vyovyote.
Amefafanua kuwa uboreshwaji huo
katika kiwanja hicho utahusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua
ndege kwa kiwango cha lami, ujenzi wa njia za maungio, ujenzi wa
maenegesho ya ndege, jengo la kisasa la abiria, ujenzi wa jengo la
kuongozea ndege, ujenzi wa kituo cha hali ya hewa na usimikaji wa taa za
kuongozea ndege
No comments :
Post a Comment