Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akinawa mikono
baada ya Uzinduzi wa Mradi Mkubwa wa Maji wenye uwezo wa kuzalisha
lita za ujazo Elfu 30 kutoka kijiji cha Rurumakilichopo kata ya
Kiomboi wilaya ya Ilamba, ikiwa ni muendelezo wa zaiara yake Mkoani
Singida.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiangalia
chanjo zilizohifadhiwa katika boksi maalum wakati alipotembelea
Hospitali ya Wilaya ya Kiomboi iliyopo wilayani Iramba katika Mkoa wa
Singida. Kushoto ni muhudumu wa chanjo Christowelo Palangyo na Dkt.
Abbas Sepoko (kulia).
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiionesha
kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Iramba (hawapo pichani) dawa za
serikali zilizo na alama maalumu ili zisiuzwe katika maduka binafsi.
Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Gwaula.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akipokea
zawadi ya mbuzi kutoka kwa Diwani wa Kinyambuli Rubeni Charles wakati
alipofanya ziara katika kijiji hicho ili kujionea hali ya ujenzi wa
kituo pamoja na utoaji huduma za afya kijijini hapo.
…………………………………………………………………………………
Na WAMJW-MKALAMA,SINGIDA
Watanzania kote nchini wametakiwa
kufuata kanuni na taratibu bora za maisha ikiwemo kubadili mfumo wa
maisha ili kuepuka kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na
udumavu kwa watoto wachanga.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine
Ndugulile katika Wilaya ya Mkalama Mkoa wa Singida wakati alipotembelea
kituo cha afya na kuongea na wananchi.
“Serikali chini ya uongozi wa
Rais Magufuli inataka kila mtanzania awe na afya bora, ndo maana
tunajitahidi kutoa elimu kwa umma kuhusiana na kutunza afya zenu ikiwemo
kufanya mazoezi na kuepuka vyakula ambavyo si salama kwa afya zetu
pamoja na kubadili mfumo mzima wa maisha”. Alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha,Naibu waziri huyo
ameendelea kusisitiza kwa upande wa akina mama walio na watoto wadogo
chini ya miaka miwili kuendelea kuwanyonyesha na kuwapa vyakula vyenye
lishe bora watoto wao ikiwa ni sehemu ya kumsaidia mtoto kukua kiakili
na kuwa na afya bora huku akisisitiza siku 1000 za mwanzo kwa mtoto
ndizo siku muhimu katika kumuwezesha kuwa na afya bora na kukua vizuri.
“Siku 1000 za mwanzo tunaanza
kuzihesabu toka mimba inapotungwa, anapozaliwa na kufikisha miaka
miwili, hiki ni kipindi muhimu sana cha mama kumnyonyesha mtoto ikiwa ni
pamoja na kumpa vyakula vyenye lishe ili mtoto aweze kuwa na afya bora
na ubongo unaofanya kazi sawa sawa”. Alisisitiza Dkt. Ndugulile.
Pamoja na hayo, Dkt. Ndugulile
amekipongeza kituo cha afya cha Kinyambuli kwa kuzitendea haki fedha
zilizotolewa na Serikali Shilingi milioni 400 ili kusaidia kupanua kituo
hicho kwa kujenga majengo mapya ya kuhudumia wagonjwa pamoja na nyumba
za watumishi.
“Nawapongeza sana wananchi wa
Kinyambuli kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa kituo hiki, ninachokiona
hapa kipo mara 300 nchi nzima, kwa kweli mnastahili pongezi na fedha za
serikali tulizoleta milioni 400 mmezitendea haki”. Alisema Dkt.
Ndugulile.
Hata hivyo Dkt.Ndugulile amesema
serikali bado ina nia kubwa ya kuboresha hali ya utoaji huduma za afya
nchini, huku ujenzi wa Hospitali kubwa ya wilaya ya Mkalama ukitarajiwa
kuanza kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Dkt. Ndugulile amesema mkoa wa
Singida umetengewa bajeti ya Bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga Hospitali
kubwa ya wilaya ya Mkalama pamoja na Singida DC.
Kwa upande wake diwani wa
Kinyambuli, Rubeni Charles ameishukuru serikali ya awamu ya tano chini
ya uongozi wa Rais John Magufuli kwa kuwakumbuka wananchi wa kijiji
hicho kwa kutoa fedha za ujenzi wa kituo kikubwa cha afya.
“Kwakweli naishukuru sana
serikali kwa kutukumbuka, wananchi wa kijiji hiki walikua wanapata shida
sana kupata huduma za afya hasa wakinamama wajawazito ambao tulipoteza
wengi kutokana na kukosa huduma hii muhimu”. Alisema Rubeni.
No comments :
Post a Comment