Wednesday, October 31, 2018

TPDC -YAJIPANGA KUONGEZA VITUO VYA KUJAZA GESI ASILIA KATIKA MAGARI PAMOJA NA KUFIKISHA MAJUMBANI NA VIWANDANI


IMG-20181031-WA0026
Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC),  Kapuulya Musomba, (wa kwanza kulia) akieleza jambo. (picha na Mwamvua Mwinyi) 
IMG-20181031-WA0028
Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo alipotembelea banda la Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC),kwenye maonyesho ya bidhaa za viwandani huko Pichandege Kibaha Pwani (picha na Mwamvua Mwinyi) 
IMG-20181031-WA0032
Msanii Afande Sele alipotembelea banda la Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC),kwenye maonyesho ya bidhaa za viwandani huko viwanja vya Sabasaba Pichandege Kibaha Pwani (picha na Mwamvua Mwinyi) 
……………………………………………………………..
NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA 
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC),  linatarajia kuongeza vituo  10 hadi 20 kwa Dar es salaam -Mtwara -Lindi, vya kujaza gesi asilia kwenye magari yaliyowekewa mfumo huo ambapo kipo kituo kimoja Ubungo ,kwa miaka kumi sasa ambacho hakikidhi mahitaji. 
Ili kufikia malengo yake ya kuongeza vituo vingi katika maeneo mbalimbali
limejipanga kuruhusu na kukubaliana na watu binafsi wenye vituo vya mafuta kuweka gesi kwenye vituo vyao .
Akitembelea maonyesho ya bidhaa za viwandani yanayoendelea viwanja vya sabasaba, Pichandege Kibaha Pwani, Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC),  Kapuulya Musomba, alisema mwamko wa watumiaji upo vizuri tatizo hakuna vituo mikoani.  
Alieleza mwaka ujao wa fedha wataongeza vituo hivyo na sasa wapo kwenye hatua ya manunuzi. 
Musomba alisema ,wataanza kuongeza vituo viwili ama vitatu Dar es salaam na kuendelea maeneo mengine, na kusema watatangaza tenda ili wawekezaji na watu binafsi  wajitokeze kufanikisha hilo. 
 “Gesi asilia ikitumika kwenye magari inaweza kupunguza zaidi ya nusu ya gharama mafuta na kuleta unafuu katika sekta ya usafirishaji nchini,
“Wadau washirikiane nasi kwa kupata ufafanuzi EWURA na TPDC ili kufanya makubaliano “alisisitiza Musomba. 
Hata hivyo alitaja mpango mwingine ni kuona wananchi wanafaidika na raslimali ya gesi lakini wanakwenda kwa awamu kulingana na fedha wanayoipata. 
“Gesi kwa ajili ya majumbani tumeanza Dar es salaam na Mtwara, na kuhusu viwandani tumeshaanza Pwani, Dar es salaam na Mtwara kwa njia ya mabomba “
Musomba alielezea,mwaka huu wa fedha kufikia 2019 watapeleka Kibaha kwa mitungi kwa kuwa mabomba hayajafika kwa kujazia Dar es salaam kisha kuwafikishia wananchi. 
Alifafanua kwa wale wa mikoa mingine wameshaanza utafiti wa kina kuona kama watoa bomba Dar es salaam, Kibaha, Bagamoyo, Chalinze, Tanga litembee kwenye mikoa kama nane na kwa kushirikiana na wadau watafikia lengo hilo. 
Nae Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo alisema TPDC ni mdau mkubwa mkoani humo kwani mkoa huo ni wa viwanda na baadhi ya wawekezaji wameanza kutumia gesi kwa matumizi yao. 
Alisema alieleza eneo jingine ni wakati ujenzi wa bandari mpya Bagamoyo ukianza watahitaji gesi kutokana na ujenzi kuambatana na viwanda vingi. 
Ndikilo alibainisha awamu ya kwanza ya ujenzi huo utaendana na ujenzi wa viwanda 190 ambapo awamu ya pili utakuwa na takriban viwanda 1,000 hivyo gesi itahitajika pia.

No comments :

Post a Comment