Dar es Salaam,
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu habari zilizochapishwa katika Gazeti la
Tanzania Daima la tarehe 26 Oktoba, 2018 toleo namba 4979 na toleo namba
4982 la tarehe 30 Oktoba, 2018 zenye vichwa vya habari “Madudu yaibuka
TRA” na “Barua za madudu TRA zavuja”. Habari inayofanana na hizi,
ilisambazwa pia katika baadhi ya Mitandao ya Kijamii ikiwa na kichwa cha
habari “PCCB Tanzania, to investigate the two tax collectors TRA and
ZRB”.
Habari hizi zinadai kuwa, Mfumo wa
Ulipaji Kodi kwa Njia ya Kielektroniki – Electronic Revenue Collection
System (e-RCS) umezimwa na kuhujumiwa na baadhi ya Maofisa wa
Serikali
kwa lengo la kujinufaisha na kuzorotesha juhudi za ukusanyaji mapato ya
Serikali.
Ukweli ni kwamba, mfumo huo
haujahujumiwa wala kuzimwa isipokuwa kuna maboresho ya kiufundi ambayo
yanaendelea kufanyika ili kuhakikisha kuwa, unakidhi malengo
yaliyokusudiwa.
Katika kipindi hiki ambacho
maboresho yanaendelea kufanyika, Kampuni za Simu pamoja na Benki
mbalimbali zinaendelea kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na hakuna
upotevu wowote wa mapato kama ilivyoripotiwa na Gazeti la Tanzania Daima
na baadhi ya Mitandao ya Kijamii.
TRA inapenda kuuhakikishia umma
kwamba, hakuna Ofisa yeyote wa Serikali mwenye nia ya kuhujumu mfumo huo
kwa lengo la kujinufaisha na kuzorotesha juhudi za Serikali za
ukusanyaji wa mapato.
Mamlaka ya Mapato Tanzania inatoa
wito kwa vyombo vya habari, wachapishaji, wahariri na waandishi wa
habari kufanya utafiti wa kina kabla ya kuandika habari na kuzingatia
weledi wakati wote wanapotimiza majukumu yao ili kuepuka upotoshaji.
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”
Imetolewa na:
Richard M. Kayombo
MKURUGENZI WA HUDUMA NA ELIMU KWA MLIPAKODI
No comments :
Post a Comment