Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akikata utepe wakati alipozindua Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya
Lushoto akiwa katika ziara ya Mkoa wa Tanga Oktoba 31, 2018. Kulia ni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu na wapili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais,
Muungano na Mazingira, January Makamba. Wapili kulia ni Mwenyekiti wa
CCM wa Mkoa wa Tanga, Henry Shekifu, watatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa
Tanga, Martine Shigela. na kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya
wilaya ya Lushoto, Ikupa Harrison Mwasyoge. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akimsikiliza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Ikupa
Harrison Mwasyoge wakati alipotembelea ofisi mpya za Halmshauri hiyo
baada ya kuzindua jengo la utawala, Oktoba 31, 2018. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akikagua ujenzi wa Soko la Kisasa la mbogamboga na matunda linalojengwa
na Serikali katika kijiji cha Malindi wilayani Lushoto, Oktoba 31, 2018.
Alikuwa katika ziara ya Mkoa wa Tanga. Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa
Tanga, Martine Shigela. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wa kijiji
cha Lukozi wilayani Lushoto wakati alipowasili kijijini hapo akiwa
katika ziara ya Mkoa wa Tanga, Oktoba 31, 2018. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Lukozi katika Jimbo la Mlalo
wilayani Lushoto akiwa katika ziara ya Mkoa wa Tanga, Oktoba 31, 2018.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya kwenye maeneo
mbalimbali nchini yakiwemo ya halmashauri ya wilaya ya Lushoto.
Amesema lengo ni kuhakikisha kila
kata inakuwa na kituo cha afya chenye uwezo wa kutoa huduma mbalimbali
muhimu zikiwemo za maabara, upasuaji na mama na mtoto.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano,
Oktoba 31, 2018) wakati akizungumza na wakananchi katika
kata ya
Malindi, baada ya kutembelea jengo la soko mbogamboga la Malindi.
Waziri Mkuu amesema Serikali
imejipanga vizuri katika sekta ya afya baada ya bajeti ya kununulia dawa
kuongezeka kutoka sh. bilioni 31 kwa mwaka na kufikia bilioni 269.
“Hatutaki tena kusikia mgonjwa
anaenda hospitali na kukosa dawa biashara hiyo tumeimaliza, Rais Dkt.
John Magufuli ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa.”
Amesema katika wilaya ya Lushoto
Serikali imetenga sh. bilioni 1.4 kwa ajili ujenzi na ukarabati wa
majengo ya vituo vya afya vya kata za Kangagai. Mnazi na Mlola.
“Halmashauri wekeni mpango
thabiti wa kujenga wodi mbili kati yake moja ya wanaume na nyingine ya
wanawake, lengo la Serikali ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi.”
Aizungumzia kuhusu mradi wa
ujenzi wa soko, Waziri Mkuu amesema mradi huo ni sehemu ya huduma
zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii nchini.
Waziri Mkuu ametaja huduma
nyingine zinazotolewa na Serikali kwa wananchi ni za afya, elimu, maji,
uchumi na ujenzi na uboreshwaji miundombinu mbalimbali ikiwemo ya
barabara.
Hivyo, amewataka wananchi watumie
vizuri soko hilo ambalo linatoa fursa kwao kufanya biashara katika
eneo zuri na kuwawezesha kuuza bidhaa zao zikiwa katika ubora.
Pia amewashauri wakulima hao
wajiunge katika vikundi na kuanzisha ushirika wao ili waweze kusaidiwa
na Serikali katika kupata mikopo kwa ajili ya kuzalisha kwa ubora zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Halmashauri ya wilaya ya Lushoto, Bibi Ikupa Mwasyoge amesema kukamilika
kwa soko hilo kutainufaisha halmashauri na wananchi.
Bibi. Ikupa amesema ujenzi wa
jengo hilo la soko la ghorofa mbili lililojengwa kwa awamu mbili ulianza
mwaka 2011 na umekamilika Septemba 2018, umegharimu sh. bilioni 1.1.
Amesema halmashauri itanufaika
kwa kupata ushuru na wananchi ambao wengi wao ni wakulima wa mboga na
matunda watakuwa na sehemu ya uhakika wa kufanyia biashara.
“Wakulima 35,000 wa kata ya
Malindi na kata jirani za Lukozi, Manolo na Shume wanaozalisha wastani
wa tani 5,900 za mboga na matunda kwa mwaka watanufaika.”
Naye, Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema Serikali
imefanya kazi kubwa katika kuboresha huduma za afya nchini.
Amesema bajeti ya dawa katika
halmashauri hiyo imeongezeka kutoka sh milioni 183 za dawa zilizokuwa
zinatolewa awani na sasa imefikia sh milioni 565.
Mbunge wa jimbo la Mlalo, Bw.
Rashid Shangazi ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kuwasaidia
wananchi wa halmashauri kuongeza thamani ya mazao yao kabla ya kuuza.
Awali,Waziri Mkuu alizindua jengo
la utawala la Halmashauri ya wilaya ya Lushoto lililogharimu sh.
bilioni 4.3. Kukamilika kwa jengo hilo kutaboresha huduma kwa wananchi.
No comments :
Post a Comment