Serikali
imetatua tatizo la kuwepo kwa karatasi za risiti zinazofutika
maandishi zinazotolewa na Mashine za Kielektroniki za kutolea Risiti
(EFDs) kwa kuwataka wafanyabiashara wote kununua karatasi hizo kwa
mawakala waliothibitishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hayo
yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge
wa Tanga Mjini Mhe. Mussa Bakari Mbarouk, aliyetaka kujua kauli ya
Serikali kuhusu risiti zinazotolewa na Mashine za EFDs kufutika
maandishi kwa muda mfupi na muda ambao utatolewa kwa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) kurekebisha hali hiyo.
Akijibu
swali hilo Dkt. Kijaji alieleza kuwa Serikali inatambua kuwa kuna
karatasi feki, lakini tatizo la kufutika kwa risiti halihitaji kutoa
muda kwa TRA wa kufanya marekebisho kwa kuwa Serikali ililifanyia kazi,
hivyo ni jukumu la wafanyabiashara kufuata maelekezo ya ununuzi wa
karatasi hizo kwa wakala waliothibitishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Naibu
Waziri Kijaji, akijibu maswali ya Msingi ya Mbunge huyo aliyetaka
kujua bei halisi za Mashine ya EFDs na kwa nini Serikali isitoe Mashine
hizo bure kwa wafanyabiashara, alisema kuwa kuna aina tano za Mashine
ambazo mfanyabiashara anaweza kununua kulingana na mahitaji yake.
“Mashine
za EFDs ni kama Rejista za kielektroniki za kodi (ETR) ambayo bei yake
ni Sh. 590,000 na hutumiwa na wafanyabiashara wasiotumia mifumo ya
Kompyuta na kihasibu na Mashine za kielektroniki zinazoweka alama/saini (Electronic Signature Devices)ambazo
hutumiwa na walipa kodi wanaotumia mifumo ya kompyuta na kihasibu, bei
yake ikiwa ni kati ya Sh. 1,000,000 hadi 1,200,000”, alieleza Dkt.
Kijaji.
Alisema kuwa Mashine nyingine ni Printa za kielektroniki za kodi (Electronic fiscal printers) ambazo
hutumia mfumo maalum wa kompyuta, bei yake ikiwa ni kati ya Sh.
1,500,000 hadi Sh. 1,700,000, pia zipo mashine ya Printa za Pampu za
Mafuta ya Petroli au Dizel (EFPP) ambazo hutumiwa na wafanyabiashara wa
mafuta, bei yake ikiwa ni Sh. 6,000,000 ikijumuisha gharama za ufungaji
na uunganishwaji kwenye pampu za mafuta.
Aidha
kuna Mashine ya Printa za Maduka ya kubadilisha Fedha za Kigeni, bei ya
mashine hizo ni Sh. 2,150,000 ikiwa ni pamoja na program ya mfumo wa software.
“Ubora
wa Mashine hizo ni lazima uthibitishwe na Mamlaka ya Mapato Tanzania-
TRA kabla mashine hizo hazijaingizwa sokoni na kuanza kutumika”,
alifafanua Dkt. Kijaji.
Dkt.
Kijaji alisema kuwa wafanyabiashara wasiosajiliwa kwenye Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) wanaponunua mashine za EFDs hulipa gharama za
ununuzi wa mashine hizo na baadae Serikali hurejesha gharama kwa
kumruhusu mlipakodi kujirejeshea fedha zake kwa utaratibu wa Input- Output tax kwenye mauzo ya mwezi husika.
Vilevile
kwa wafanyabiashara wasiosajiliwa kwenye VAT na wanaoandaa hesabu za
mizania, hujirejeshea gharama za ununuzi wa mashine kwa kuingiza gharama
husika kama gharama za kuendesha biashara kwa mujibu wa sheria ya Kodi
ya Mapato.
Naibu
Waziri huyo amebainisha kuwa, kwa wafanyabiashara wasioandaa hesabu za
mizania wanajirejeshea gharama za mashine kwenye kiasi cha kodi
walichokadiriwa kwa mwaka husika na iwapo hawatakuwa wamejirejeshea kwa
asilimia miamoja, kiasi kilichobakia kitasogezwa mwaka unaofuata.
No comments :
Post a Comment