NALILIAN LUNDO -
MAELEZO, DODOMA.
SERIKALI imetoa kibali
cha kuajiri watumishi wapya 15,000 ili kuziba pengo lililosababishwa na
kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara watumishi wa Umma waliobainika
kughushi vyeti.
Hayo yameelezwa leo
Bunge, Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Manejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Capt. (Msataafu) George Mkuchika (pichani) alipokuwa akijibu
swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Aida Khenani kuhusu mkakati wa Serikali wa
kuziba nafasi zilizoachwa wazi na watumishi waliokumbwa na sakata la vyeti
feki.
"Vibali vya
kuajiri watumishi hao vimetolewa katika ngazi ya Wizara, Idara zinazojitegemea,
Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Waajiri wote
wameendelea kujaza nafasi hizo, " alisema Mhe. Mkuchika.
Vilevile, amesema Serikali
imetoa vibali vya ajira kwa Mamlaka zote za Serikali za Mitaa Kumb. Na.
CFC.26/205/01/PF/91 cha tarehe 22 Agosti, 2017 na kibali Kumb. Na
CFC.26/205/01/GG/95 cha tarehe 12 Machi, 2018 kuziba nafasi zote za Watendaji
wa Vijiji na Mtaa zilizoachwa wazi kutokana na zoezi la kuhakikiwa vyeti kwa
kuajiriwa watumishi wapya.
Aidha, amesema katika
mwaka wa fedha 2017/2018 kwa kutambua umuhimu kwa kuajiri watumishi wa kada
mbalimbali Serikali imetoa vibali vya kuajiri watumishi 22, 150 wakiwemo
watumishi wa kada za Ualimu 6,840, Fundi Sanifu wa Maabara za shule 160, kada
za Afya 8,000, Wahadhiri wa Vyuo Vikuu 624 na watumishi 6,526 wa kada nyingine.

No comments :
Post a Comment