NA LILIAN LUNDO - MAELEZO, DODOMA.
SERIKALI imetoa wito kwa wazazi/walezi na wote wenye jukumu la
kutoa malezi na matunzo kwa watoto kuhakikisha wanatimiza wajibu wao
kikamilifu.
Wito huo umetolewa leo, Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa
Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine
Ndugulile alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Amina Nassor
Makilagi kuhusu mkakati wa Serikali wa kuweka sheria kali itakayowabana wazazi
ambao wamekuwa wakitelekeza watoto na familia zao.
"Matunzo, malezi na ulinzi wa mtoto ni haki ya mtoto kwa
mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009. Aidha kifungu cha 7 - 9 kinatoa
majukumu kwa mzazi/mlezi na mtu yeyote mwenye jukumu la kumlea mtoto
kuhakikisha anawatunza na kuwalea watoto, ikiwemo kuwapatia huduna zote muhimu,
kama chakula, malazi, mavazi, elimu na kuwalinda na vitendo vya unyanyasaji,
ukatili, unyonyaji na utekelezaji," alisema Dkt. Ndugulile.
Ameendelea kusema kuwa kifungu cha 14 cha Sheria ya Mtoto
kinatoa adhabu kwa mzazi/mlezi yeyote atakayekiuka kifungu hiki atatozwa faini
isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kisichozidi miezi sita au vyote
viwili kwa pamoja.
Vile vile amesema, kwa kipindi cha 2016/2017 jumla ya mashauri
6557 yanayohusu matunzo na malezi ya watoto na wanawake yalishughulikiwa katika
ngazi ya Mamlaka za Halmashauri na Serikali za Mitaa.
Aidha, Dkt. Ngugulile amezitaka familia zilizotelekezwa kutoa
taarifa kwenye ofisi za Ustawi wa Jamii zilizoko katika Halmashauri wanazoishi
ili mashauri yao yaweze kusikilizwa na watoto kupata huduma stahiki kwa ajili
ya makuzi yao.
Pia ametoa wito kwa Maafisa Ustawi wa Jamii katika ngazi zote za
Serikali kuhakikisha wanashughulikia kwa haraka mashauri yanayowasilishwa
kwenye ofisi za kwa kutumia sheria na taratibu zilizopo.

No comments :
Post a Comment