Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt.Philip Isdor Mpango (Mb), akiongea na wafanyabiashara wa Mkoa wa
Tanga alipokutana na wafanyabiashara hao katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa
wa Tanga, kusikiliza maoni na changamoto zinazowakabili katika masuala
ya kodi.
Mkuu wa Wilaya ya
Tanga Mh.Thobias Mwilapwa akiwahutubia wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga
kabla ya Kumkaribisha Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango (Mb) kuzungumza na wafanyabiashara hao katika Mkutano
uliofanyika kwenye ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Baadhi ya
wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga wakifuatilia kwa makini hotuba ya
Waziri wa Fedha na Mipango, Mh. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), alipokuwa
akizungumza na wafanyabiashara hao Jijini Tanga kuhusu kuimarisha
ushirikiano kati yao na Serikali ili kuliletea maendeleo Taifa.
Meneja wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga, Bwana Masawa Masawa (Kushoto),
akiwa na Naibu Kamishna wa Forodha, Bwana Qamdijay Akonaay (Kulia),
wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mh. Dkt. Philip Isdor
Mpango (Mb) (hayupo pichani) wakati wa mkutano na wafanyabiashara
uliofanyika Jijini Tanga.
Maafisa wa
Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
(waliokaa mbele) wakiwa katika mkutano wa Waziri wa Fedha na Mipango na
wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga.
Katibu wa Waziri
wa Fedha na Mipango, Bwana Edwin Makamba akifuatilia na kuchukua
kumbukumbu za mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango na
wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga uliofanyika Jijini Tanga katika ukumbi
wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa.
Na Benny Mwaipaja, WFM, Tanga
WAZIRI wa Fedha
na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amekutana na wafanyabiashara mkoani
Tanga na kuwaeleza kuwa Serikali imeanza kulipa madai ya marejesho ya
kodi ya Ongezeko la thamani (VAT Refund) kwa kampuni na wafanyabiashara
mbalimbali nchini wakiwemo waagizaji wa sukari za viwandani ambao madai
yao yamehakikiwa kuanzia mwezi huu wa Septemba, 2018.
Kauli hiyo ya
Serikali inafuatia maombi ya wafanyabiashara wa mkoa huo walioitaka
Serikali kuwalipa wafanyabiashara wanaodai kurejeshewa fedha zao
zinazotokana na kufanya biashara zao nje ya nchi pamoja na wazabuni
mbalimbali.
Waziri Mpango
amesema kuchelewa kulipwa kwa madai hayo kunatokana na kuwepo kwa
udanganyifu mkubwa kwa baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu
hivyo kutaka kuingizia Serikali hasara kwa kulipa madai hewa. ‘Kuna
baadhi ya wafanyabiashara sio waaminifu, mfano tulipofanya uhakiki
tuligundua madai hewa ya pembejeo ya zaidi ya Shilingi bilioni 87’, alisema Waziri Mpango.
Dkt. Mpango
aliwahakikishia wafanyabiashara wote nchini kuwa serikali itahakikisha
inaweka mazingira mazuri ili kila mwananchi mwenye nia njema aweze
kufanya biashara halali itakayomletea faida na serikali iweze kukusanya
kodi bila ya kumuonea mtu.
Awali Mwenyekiti
wa wafanyabiashara Mkoa wa Tanga Bw. Deogratias Ruhinda, alisema kuwa
wafanyabiashara hasa wakulima wa zao la Mkonge wanakutana na changamoto
kubwa kutokana na serikali kuruhusu na kutoa msamaha wa baadhi ya kodi
kwa wafanyabiashara wanaoingiza Kamba za manila hapa nchini, hivyo
kulifanya zao la mkonge kutokuwa na soko hapa nchini kutokana na bei ya
Kamba hizo za nje kuwa chini ukilinganisha na Kamba zinazotokana na
mkonge.
Aidha
wafanyabiashara hao waliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza
kina cha Bandari ya Tanga ili meli kubwa ziweze kuja katika bandari
hiyo na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kwenda nje ya nchi
tofauti na ilivyo sasa ambapo bidhaa nyingi kutoka Tanga zinasafirishwa
kwa kutumia Bandari ya Dar es Salaam au Mombasa jambo linalowaongezea
gharama kubwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga.
Akijibu hoja
mbalimbali za wafanyabiashara hao, Dkt. Philip Mpango, aliwahakikishia
kuwa Serikali itazipitia na kuzitolea ufafanuzi kero zote zinazohusu
kodi ili kurahisisha biashara na kuweka mahusiano mazuri kati ya
wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania, hali ambayo itaongeza
mapato kwa serikali. Pia amesema Serikali inalifanyia kazi suala la
wingi wa kodi anazolipa mfanyabiashara kwa Taasisi mbalimbali za
serikali ili kodi hizo ziweze kutozwa sehemu moja na kupunguza adha
wanazopata walipa kodi.
Waziri Mpango
aliwataka wafanyabiashara hao kutosita kuishauri serikali njia bora ya
kukusanya kodi na kutoa maoni yao jinsi ya tozo mbalimbali zinazotozwa
na serikali kwa kuiandikia Mamalaka ya Mapato Tanzania au Wizara ya
Fedha na Mipngo ili serikali iweze kuboresha maeneo yenye mapungufu kwa
faida ya Taifa. Pia Mh.Waziri amewataka wafanyabiashara kote nhini
kushiriki katika mikutano ya sera za kodi inayondaliwa na Wizara ya
Fedha na Mipango ambayo huanza mwezi Disemba hadi Januari kila Mwaka.
No comments :
Post a Comment