Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan
Na Mwandishi Wetu,
MAELEZO
DAR ES SALAAM
28.9.2018
MAKAMU wa Rais,
Samia Suluhu Hassan amezitaka Wizara, Wakala, Idara, Taasisi za Serikali
zinazohusika na sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, maliasili na utalii na
Serikali za Mitaa kuandaa mipango na mikakati ya pamoja ili kupunguzia
gharama kwa Serikali katika
kukabiliana na changamoto ya kuenea kwa
viumbe wageni/vamizi nchini.
Akizungumza
katika hafla ya uzinduzi wa kikosi kazi kutoka Taasisi za Umma
watakaojikita katika kutatua changamoto za viumbe wageni/vamizi leo
Jijini Dar es Salaam, Mhe. Samia alisema wakati umefika kwa Wataalamu wa
Wizara, taasisi, wakala za Serikali kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza
kudhibiti athari za viumbe wageni/wamizi ambao wameanza kuleta athari za
kijamii na kiuchumi nchini.
Makamu wa Rais
alisema kwa mujibu wa Taasisi ya Global Invasive Species Database,
Tanzania ina takriban aina 100 za viumbe Vamizi/Wageni wakiwemo wadudu
wa magonjwa ya mimea, wadudu, magugu ya kwenye maji na magugu ya nchi
kavu, wanyama na miti.
Mhe. Samia
alisema Sekta na Taasisi zote hazina budi kufanya kazi kwa pamoja kwa
kupeana taarifa na mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo pamoja
na ushirikishwaji wa wadau wote zikiwemo Halmashauri, Asasi za Serikali
na zisizo za Serikali, Sekta binafsi na wananchi ili kuwa na uelewa wa
pamoja wa kutafuta ufumbuzi.
“Zamani ulikuwa
unakuta Taasisi Fulani inaandika mradi wa mazingira mfano magugu maji,
fedha wanazoomba wanatumia wao, na wengine pia wanatekeleza mradi
huohuo, umefika wakati sasa kwa taasisi hizi kufanya kazi pamoja ili
kuipunguzia gharama Serikali” alisema Samia.
Aidha Samia
alisema uharibifu wa makazi ya viumbe asili ndio chimbuko la uwepo wa
Viumbe Wageni/Vamizi ambapo shughuli za kibinadamu zinatajwa kuwa ndiyo
sababu kuu ya uharibifu/ubadilishaji wa makazi asili ya viumbe.
Anaongeza kuwa
katika mkataba wa Kimataifa wa Bioanuai ambao Tanzania imeuridhia,
unataja kuwa viumbe wageni/vamizi ni sababu ya pili inayosababisha
uharibifu wa makazi ya viumbe asili na hata kusababisha kutoweka kwa
viumbe hao wa asili.
Akifafanua zaidi
alisema kuenea kwa viumbe hao wameleta na wanaendelea kuleta madhara
makubwa katika mazingira hususan kuharibika kwa mifumo ikolojia, upotevu
wa bioanuai, na baadhi ya viumbe hao ni sumu hivyo huleta madhara
ikiwemo vifo.
Kwa mujibu wa
Samia alisema viumbe hao pia wamesababisha baadhi ya wanyama ambao
walikuwa kivutio kwenye mbuga za wanyama kuhama kwenye maeneo yao ya
asili jambo linalosababisha wanyama hao kutoonwa tena na watalii, ambapo
baadhi yao huingia kwenye maeneo ya makazi ya watu na hivyo kuuliwa
kirahisi.
“Kwa mfano,
nimejulishwa kuwa katika Hifadhi ya Ngorongoro, takribani theluthi moja
ya eneo la shimo ambapo ndipo wanyama wanapata malisho yao, limevamiwa
na viumbe hawa na linaendelea kuvamiwa” anasema Samia.
Kwa upande wake,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January
Makamba alisema Serikali imeipatia hadidu rejea nane kikosi kazi hicho
ili kuweza kubaini ukubwa, athari na changamoto za viumbe hao ambao
tayari wameanza kuleta athari za kijamii na kiuchumi katika maeneo
mbalimbali nchini.
“Nilifanya ziara
katika hifadhi ya Bonde la Ngorongoro na nilibaini kupungua kwa wanyama
katika hifadhi hiyo pamoja na kumea kwa majani kwa ajili ya malisho ya
wanyama nilielezwa na wataalamu kuwa majani hayo ni mimea vamizi ambayo
ni sumu kwa wanyamapori, hivyo kikosi kazi hiki tumewapa maelekezo ya
kuja na majibu kuhusu suala hili”.
Waziri Makamba
alisema mbali na athari zilizoanza kujitokeza katika hifadhi ya Bonde la
Ngorongoro, maeneo mengine yaliyoanza kuathiriwa na viumbe
wageni/vamizi hao ni pamoja na Ziwa Jipe lililopo Wilayani Simanjiro
Mkoani Manyara na pamoja jamii ya mimea ya maua yaliyoanza kuota katika
maeneo ya Kibaigwa Mkoani Dodoma.
Naye Waziri wa
Kilimo, Dkt. Charles Tizeba aliwataka wajumbe wa kikosi kazi hicho
kutambua kuwa suala la mazingira ni la usalama wa taifa, hivyo ni wajibu
wao kufanya kazi kwa uadilifu na kuleta majawabu yatayoweza kutatua
changamoto hiyo katika miaka mingi zaidi.
Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos
Silayo alisema mtawanyiko wa viumbe wageni/vamizi wanasambishwa zaidi na
shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabia nchi ambapo mifano
michache iliyopo Tanzania kwa sasa ni pamoja na uwepo wa magugu maji,
mti wa mrashia na upandikazaji wa mazao ya mimea na mifugo.
No comments :
Post a Comment