Wednesday, September 19, 2018

NHIF TABORA YALIPA BILIONI 3.8 KWA WATOA HUDUMA MKOANI HUMO KATIKA MWAKA WA FEDHA ULIOPITA


4 (16)
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri(wa pili kutoka kushoto) akifungua mkutano wa wadau wa afya hivi karibuni mkoani humo. Wengine ni  Katibu Tawala Mkoa huo Msalika Makungu( kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Tabora Komanya Kitwala(wa pili kutoka kulia) na  Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Gunini Kamba(kulia)

3 (20)
Kaimu Katibu wa Afya Mkoa wa Tabora Tausi Yunge akitoa takwimu za wanawake waliojifungua tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa wakati wa mkutano wa wadau wa afya mkoani humo.
2 (22)
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Gunini Kamba akitoa mada kuhusu hali ya huduma ya afya mkoani humo  hivi karibuni wakati wa mkutano wa wadau wa afya.
1a (1)
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa wadau wa afya mkoani Tabora wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tabora (hayupo katika picha ) wakati wa ufunguzi wa mkutano huo hivi karibuni.
NA TIGANYA VINCENT
RS TABORA
19 September 2018
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) Mkoa wa Tabora umelipa jumla ya bilioni 3.8 kwa watoa huduma mbalimbali mkoani humo katika mwaka wa fedha uliopita.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Jacob Mwailubi wakati wa mkutano wa wadau wa afya wa Mkoa huo.
Alisema vituo vya Serikali vimelipwa bilioni 1.021 , watoa huduma wa binafsi bilioni
1.246 na Vituo vya Taasisi za dini vimelipwa kiasi bilioni 1.566.
Aidha Mwailubi alisema NHIF mkoani humo imefanikiwa kusajili wanachama wapya 3,063 katika mwaka wa fedha uliopita na kuufanya ufikishe wanachama  20,400.
Mwailubi alisema kati yao watumishi wa umma ni 16,938, Mashirika binafsi 307, wastaafu 175, Vyuo vya Elimu ya juu 2,131, Madiwani 268,Viongozi madhehebu ya dini 125, Wanachama binafsi 6 na Watoto chini ya miaka 18 ni  450.
Aidha alisema katika kipindi hicho Ofisi ya Mkoa ya NHIF iliweza kukusanya jumla ya milioni 645.9 kama michango ya wanachama  ambapo kati yake  milioni 325.3 ni michango toka taasisi za umma wakati milioni 320.6 ilikusanywa kutoka mashirika binafsi.
Hata hivyo alisema Halmashauri za Wilaya ya Tabora –Uyui, Igunga na Urambo hazijalipa malimbikizo ya michango ya Watumishi wanaolipwa kupitia mapato ya ndani ya jumla milioni 39.5.
Mwailubi alisema Halmashauri ya wilaya Tabora  inadaiwa shilingi milioni 1.6, Igunga milioni 28.2 na Urambo milioni 8.6.
Aliwahimiza michango hiyo ilipwe ili watumishi husika wapate huduma za matibabu.
Wakati huo huo Mwailubi alisema NHIF imesajili jumla ya Vituo vya Huduma za Afya  302 ambapo kati ya hivyo  vituo 243  vinavyomilikiwa na serikali, vituo 24 ni Taasisi na mashirika yasio ya serikali na  vituo 35 vinavyomilikiwa na watu binafsi yakiwemo maduka ya dawa.

No comments :

Post a Comment