Na Felix Mwagara, MOHA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Kangi Lugola amewataka viongozi na watumishi mbalimbali wa wizara yake
wafanye kazi kwa kushirikiana na kuacha tabia ya kunyanyasana wakati
wanatekeleza majukumu yao ya kikazi.
Lugola pia amesema kila mtumishi
wa wizara yake ana umuhimu mkubwa kwa kufanikisha mafanikio ya wizara
hiyo kwakuwa watumishi hao wanafanya kazi kwa kutegemeana.
Akizungumza na watumishi wa makao
makuu wa wizara hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Veta, jijini
Dodoma jana, Lugola alisema kikao hicho alikiitisha kwa lengo la kujuana
na watumishi hao pamoja na kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili
wafanyakazi.
“Mambo muhimu ambayo yatatuletea
mafanikio ndani ya wizara yetu ni kufanya kazi kwa bidii, kufanya kazi
kwa kushirikiana na tukifanya hivyo hakika tutapendana na kuzidi
kufanikiwa,” alisema Lugola.
Lugola aliongeza kuwa, hapendi
kuona mtumishi yeyote ananyanyaswa kwa kutopewa haki zake au
kucheleweshewa pasipo kuwa na sababu za msingi ikiwemo malipo mbalimbali
ya watumishi wanayodai, na endapo yatatokea hayo watumishi hao wamletee
kero zinazowakabili ofisini kwake na kwa kushirikiana na katibu mkuu wa
wizara hiyo watazitatua.
“Utumishi wa umma naujua, na pia
nimepitia manyanyaso kadhaa mpaka leo nimefikia hapa kutokana na
historia yangu, kwanini tusipendane?, kwanini tunyanyasane?, kwanini
tusishirikiane?, ni tabia mbaya na inatakiwa kulaaniwa kwa baadhi ya
wakuu wa idara na vitengo pamoja na wengineo ambao wanatabia ya
kunyanyasa watumishi waliochini yao,” alisema Lugola.
Mkutano huo ambao ni wa kwanza kwa
Waziri Lugola, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali, Jacob Kingu
pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Ramadhan Kailima, kuzungumza na watumishi
wa Wizara hiyo tangu walipoteuliwa miezi kadhaa iliyopita, walitaka
kujuana zaidi na watumishi wa wizara hiyo pamoja na kujua changamoto zao
zinazowakabili.
Aidha, Katibu Mkuu, Meja Jenerali
Kingu, kwa upande wake aliwataka watumishi wa wizara yake kupendana na
kutengeneza umoja wa kusaidiana katika matukio mbalimbali yakiwemo ya
furaha na matatizo.
“Anzisheni umoja, mpendane,
mshirikiane katika matukio mbalimbali, wekeni utamaduni ya kuchangiana,
hii itasaidia sana kufanya kazi kwa umoja na kupata mafanikio zaidi,”
alisema Meja Jenerali Kingu.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo, Ramadhan Kailima alisema katika maisha yake anachukua unyanyasaji
wa watumishi na wa aina yoyote, hivyo hatakubaliana na kiongozi yeyote
atakaye mnyanyasa mtumishi.
“Tufanye kazi vizuri bila
kunyanyasana, wanaojijua wanatabia hizo wajirekebishe tuweze kufanya
kazi kwa upendo, anayedai haki zake apewe kwa mujibu wa utaratibu, sisi
ni viongozi na moja ya kazi zetu ni kutokuaona mtumishi yeyote
ananyanyaswa,” alisema Kailima.
No comments :
Post a Comment