Sunday, September 23, 2018

MAAFISA BIASHARA WATAKIWA KUJIKITA KATIKA UTOAJI WA ELIMU ILI KUBORESHA MAKUSANYO YA SERIKALI


  Mkuu wa Wilaya ya Uyui Gift Msuya akitoa ufafaunizi hivi karibuni wakati warsha ya utetezi wa majadiliano  katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji iliyowahusisha viongozi wa Serikali na sekta binafsi mkoani hapa.

NA TIGANYA VINCENT-RS TABORA

MAAFISA Biashara Mkoani Tabora wametakiwa kujitahidi kuwatembelea wafanyabiashara na kutoa  elimu ambayo itawasaidia kutambua wajibu wao wa kulipa kodi mbalimbali kwa hiari ili kuboresha makusanyo ya mapato ya Serikali kwa ajili ya maendeleo ya Nchi.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Ingembensabo Emmanuel Malunde wakati akifunga warsha ya utetezi majadiliano  katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji iliyowahusisha viongozi wa Serikali na sekta binafsi mkoani hapa.

Alisema kuwa baadhi ya Maafisa hao wamekuwa wakijikita katika kukusanya mapato bila kutoa elimu kwa wadau wao juu ya uendeshaji wa biashara kwa tija na umuhimu wa wao kulipa kodi na ushuru wa Serikali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Malunde alisema ukosefu wa elimu wakati mwingine ndio umekuwa ukisababisha wafanyabiashara kuvutana na Watendaji wa umma wa sekta ya biashara bila sababu za msingi.

Alisema elimu ya kutosha itawezesha kujenga urafiki kati yao na watendaji wa umma na hivyo kufanya mazingira ya ukusanyaji kodi  kuwa rahisi na kuondoa dhana ya baadhi ya kuona kama wananyanyaswa na Maafisa Biashara.

Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo Mhasibu Mkuu (CA) wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku Kanda ya Magharibi(WETCU) Goodluck Amos alisema Maafisa Biashara ni lazima watambue kuwa kila wakati kunatokea mabadiliko katika teknolojia na uboreshaji wa mifumo ya ukusanyaji mapato ambayo pia wafanyabiashara wanapaswa kuelimishwa kila wakati kunapokuwepo na mabadiliko.

Alisema hatua hiyo itawasaidia wao kwenda na wakati na kuachana na mtindo wa kizamani wa kulipa mapato ya Serikali kwa ajili ya kuwa na mazingira ambayo ni rafiki ya ulipaji wa kodi za Serikali.

Amos alisema wasipatiwa elimu ya kutosha baadhi yao wanaweza kuendelea na mtindo wa kufanyabiashara ambayo haina tija kwao na Serikali.

Warsha hiyo ya siku mbili iliandaliwa na Taasisi ya Wafanyabiashara , Viwanda na Kilimo(TCCIA) Mkoa wa Tabora kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es salaam shule ya Biashara kwa lengo kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa viongozi wa Serikali na sekta binafsi mkoani hapa.

  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Haruna Kasela akitoa maelezo kwa niaba yahivi karibuni wakati warsha ya utetezi wa majadiliano  katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji iliyowahusisha viongozi wa Serikali na sekta binafsi mkoani hapa.


Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Ingembensabo Emmanuel Malunde  akifunga hivi karubuni warsha ya utetezi majadiliano  katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji iliyowahusisha viongozi wa Serikali na sekta binafsi mkoani hapa.

No comments :

Post a Comment