Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe, na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka wakikagua kokoto zitakazotumika katika ujenzi
wa barabara ya Maswa-Bariadi yenye urefu wa KM 49.7 kwa kiwango cha lami,
Mkoani humo.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe, akifafanua jambo kwa
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka
wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Maswa-Bariadi yenye
urefu wa KM 49.7 kwa kiwango cha lami, Mkoani humo.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe, akioneshwa na Meneja
wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Simiyu Mhandisi Albert Kent, kazi zinazoendelea
katika ujenzi wa daraja la mto Simyu, wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa
ujenzi wa barabara ya Maswa-Bariadi yenye urefu wa KM 49.7 kwa kiwango cha
lami, Mkoani humo.
UJENZI unaondelea
wa barabara ya Maswa-Bariadi yenye urefu wa Km 49.7 kwa kiwango cha lami
unatarajiwa kufungua mkoa wa Simiyu na mikoa jirani ya Mara, Mwanza na Shinyanga hivyo kutarahisisha usafirishaji wa abiria na
mizigo.
Kauli hiyo
imetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe
mkoani Simiyu wakati akikagua barabara hiyo inayojengwa na mkandarasi wa
kampuni ya CHICO na kuridhishwa na hatua zilizofikiwa katika ujenzi huo toka
ulipoanza mwezi Oktoba mwaka 2017.
"Nimeridhishwa
na hatua zilizofikiwa na nina imani mkandarasi atamaliza mapema mradi huu",amesisitiza
Waziri Kamwelwe.
Aidha,
ameupongeza uongozi wa mkoa huo na Wakala wa Barabara (TANROADS), kwa kusimamia
mradi huo usiku na mchana na kuwataka kutoa taarifa muda wowote endapo kutakuwa
na changamoto zinazoweza kukwamisha mradi huo.
Akizungumzia
kuhusu Kiwanja cha Ndege cha Simiyu, Mhandisi Kamwelwe amemueleza Mkuu wa
Mkoa kuwa hatua za awali zinaendelea
katika kuhakikisha kiwanja hicho kinajengwa ili kufungua mkoa huo katika sekta
za usafirishaji na uwekezaji.
Kwa upande
wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, ameishukuru Serikali kwa kujenga
kipande cha barabara hiyo baada ya ile ya Mwigumbi-Maswa kukamilika kwa kiwango
cha lami kwa kuwa imekua ni kichocheo cha kuunganisha nchi yetu na nchi za
maziwa makuu ambazo ni Uganda, Burundi, Rwanda, Kenya na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo(DRC).
Naye,
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Simiyu Mhandisi Albert Kent amemueleza Waziri huyo
kuwa mradi huo mpaka sasa umefikia asilimia 20 na unatarajiwa kukamilika
ifikapo mwezi Oktoba mwaka 2019.
Mhandisi
Kent ameongeza kuwa kazi zilizofanyika mpaka sasa ni mkandarasi kuanza ujenzi
wa madaraja makubwa mawili ya Banhaya na Simiyu na ameshamaliza kujenga
madaraja madogo 9 kati ya 12 na makalvati 36 kati ya 58.
Mradi wa Maswa-Bariadi
unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 na
unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi Bilioni 86. Kukamilika kwa mradi huo kutakamilisha
ujenzi wa barabara ya Mwigumbi-Maswa-Bariadi-Lamadi yanye jumla ya urefu wa KM
171.8.
No comments :
Post a Comment