Saturday, August 18, 2018

ZSSF yatoa msaada katika Hospitali ya Mnazimmoja

Naibu waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Harusi Saidi Suleiman ameushukuru uongozi wa Mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar ZSSF kwa kutoa msaada wa vitanda, Mashuka na vifaa vya kufanyia usafi katika hospitali ya Mnazimmoja ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za kutimiza miaka 20 ya mfuko huo. Mhe. Naibu waziri Harusi ametoa shukuruni kwa niaba ya uongozi mzima wa wizara ya afya mbele ya Mkurugenzi mwendeshaji wa ZSSF Ndg. Sabra Issa Machano wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo katika jengo jipya la Hospitali ya Mnazimmoja.

Amesema bado hospitali inakabiliwa na uhaba wa baadhi ya vifaa huku akikiri baadhi ya wagonjwa  kulazwa chini kutokana na uhaba huo.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mnazimmoja Dkt. Ali Salum Ali amesema si mara ya kwanza kwa ZSSF kuiunga mkono hospitali hiyo amewashukuru kwa kuwakumbuka kwa mara nyengine tena huku akisema wamefarijika sana kupokea msaada huo na watahakikisha vifaa hivyo vinatumika Hospitali kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF Ndg. Sabra amesema dhamira ya msaada huo ni kusaidia jitihada za Serikali na Hospitali ya Mnazimmoja ambayo kwa siku huzalisha Watoto 100 ili kuona inatoa huduma bora ya Afya kwa jamii.
ZSSF imekabidhi msaada wa Vitanda vya kulalia wagonjwa 13 na magodoro yake, Mashuka 89 na vifaa vya kufanyia usafi ambapo jumla ya Gharama za vitu vyote hivyo ni Tsh. Milioni 15.

No comments :

Post a Comment